Licha ya kucheza jana, Kessy bado hakijaeleweka
LICHA ya kuruhusiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, beki wa zamani wa Simba, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, bado hakijaeleweka kuichezea Yanga msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom, Tanzania Bara.
Kessy alisajiliwa na Yanga katika dirisha dogo la Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho, lakini alishindwa kuitumikia kutokana na alikuwa bado ana mkataba na Simba.
Hata hivyo, Simba waliweka pingamizi TFF huku wakidai fidia ya Sh milioni 126 kwa madai Kessy kuvunja mkataba kwa kuanza kuitumikia Yanga kabla ya kumalizika kwa mkataba wake na Wekundu wa Msimbazi hao.
Akizungumza na BINGWA jana, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema mchezaji huyo aliruhusiwa kucheza mchezo huo, lakini hataruhusiwa Ligi Kuu mpaka suala lake litakapojadiliwa na Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho hilo.
“Kessy ameruhusiwa kucheza mechi ya Ngao ya Jamii kwa kuwa si ya ligi, lakini suala lake bado lipo pale pale mpaka kamati itakapokutana na kutoa uamuzi,” alisema Lucas.
Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Jonas Kiwia, alitoa ruhusa ya kucheza mchezaji huyo.
Post a Comment