UONGOZI wa klabu ya Simba umekata mzizi wa fitina juu ya straika wao wa kimataifa Mrundi, Laudit Mavugo, baada ya kuanza mazungumzo na klabu iliyomlea na kukuza kipaji chake cha soka (Solidarity) ya nchini kwao.
Simba imemsajili mchezaji huyo na kumpa mkataba wa miaka miwili akitokea Vital’O ambapo zilienea taarifa kuwa Wekundu hao wa Msimbazi wanaweza wasimtumie kutokana na kutomalizana na Vital’O pamoja na timu hiyo iliyomlea lakini sasa mambo yanakwenda vizuri.
Taarifa kutoka nchini Burundi zinadai kuwa Mavugo alikuwa akiichezea Vital’O kwa mkopo wa miaka miwili akitokea kwenye timu hiyo ya Solidarity na mkataba huo ulishamalizika hivyo tetesi kwamba bado ni mali ya Vital’O hazina ukweli wowote.
DIMBA lilipomtafuta Mavugo alisema hana mkataba na Vital’O ila kuna vitu ambavyo viongozi wa klabu ya Simba wanatakiwa kuviweka sawa ili mambo yamalizike kwa amani huku akisisitiza kuwa ni mali halali ya Simba.
“Hayo ni maneno tu, sina mkataba na Vital’O, nimeondoka Burundi nikiwa mchezaji huru, nadhani kuna vitu vidogo vidogo ambavyo labda Simba wanatakiwa kuvimalizia lakini si kwamba nina mkataba nao,” alisema.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope, alisema Mavugo ni mchezaji wao halali na wako katika hatua za mwisho za kumalizana na Solidarity kwa ajili ya kumtumia msimu ujao.
“Kwa sasa Mavugo ni mchezaji wetu halali, tulifuatilia chama cha soka nchini humu tukagundua kwamba mchezaji huyo ametokea katika timu ya Solidarity na Vital’O walimsajili kwa miaka miwili kwa mkopo, tumefika hadi kwenye shirikisho lao, tumehakikisha kwamba Solidarity ndio wenye mchezaji,” alisema.

Post a Comment

 
Top