KOCHA wa West Ham United, Slaven Bilic, amesema straika wa Chelsea, Diego Costa, alistahili kadi nyekundu kwenye mechi ambayo West Ham walichapwa 2-1 na Chelsea juzi usiku huko Stamford Bridge.
Costa ndiye aliyefunga bao la pili na la ushindi kwa Chelsea katika dakika ya 89.
Lakini, kabla ya hapo, akiwa tayari amelimwa kadi ya njano, Costa alimchezea rafu kipa wa West Ham, Adrian, lakini mwamuzi Anthony Taylor alitoa adhabu bila kumpa kadi ya pili ya njano ambayo ingezaa nyekundu na kutolewa nje.


Kubaki kwa Costa uwanjani kulimfanya ampe kocha wao mpya, Antonio Conte ushindi wao wa kwanza katika mechi yao ya kwanza ya msimu mpya wa Ligi Kuu England.
Akizungumza na Sky Sports, Bilic alisema: “Tayari alikuwa na kadi na alicheza rafu na sidhani ni kusudi, lakini alichelewa na alipaswa kupewa kadi nyingine.”
Katika mechi hiyo, West Ham walipata pigo baada kulazimika kumtoa nje mchezaji wao mpya kutoka Ghana, Andre Ayew, aliyeumia pajani katika dakika ya 35.

Post a Comment

 
Top