TIMU ya taifa ya Nigeria imekuwa na maisha kama ya maigizo katika michezo ya Olimpiki ambayo inaendelea nchini Brazil kwa kuwa kila tukio lao limeonekana kama jambo la kushangaza.

Kwanza timu hiyo ilichelewa kuwasili nchini Brazil kutokana na masuala ya tiketi za ndege kutokuwa katika utaratibu mzuri, hali iliyosababisha timu hiyo kukosa muda mzuri wa kufanya mazoezi na kujiandaa.

Lakini baada ya kuwasili Rio de Janeiro na kutokuwa na muda mrefu wa mapumziko Nigeria ilicheza na Japan ambapo kabla ya mchezo kuanza, waratibu wakakosea na kuweka wimbo wa taifa tofauti na ule wa Nigeria jambo ambali lilisababisha Wanigeria wenyewe wabaki midomo wazi.

Lakini pamoja na matukio yote hayo, bado Nigeria ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 5-4 dhidi ya Japan.

Imeelezwa kuwa sababu za kuchelewa ndege ni kutokana na masuala ya fedha katika malipo ya tiketi hasa kutoka kwa mamlaka husika zinazosimamia soka la nchi hiyo.

Hii siyo mara ya kwanza kwa Nigeri au timu za Afrika kuwa na maisha tata katika michuano hiyo mikubwa. Mwaka 2014, timu ya Cameroon ilichelewa kuwasili katika Kombe la Dunia kutokana na wachezaji kugoma kwa kuwa hawakulipwa posho zao.

Post a Comment

 
Top