WAKATI Yanga ikiwa katika hatua za mwisho kucheza
mechi yake ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mo Bejaia, wachezaji wa Yanga
wamelalamika kushinikizwa na baadhi ya wanachama wanaodai wanatokea katika
matawi ya Yanga.
Wachezaji
saba wa Yanga, wamezungumza na gazeti hili na kulalamika kuwa wamechukizwa na
shinikizo kutoka kwa baadhi ya watu wanaojiita wanachama wanaotaka kuwavuruga
wakiwataka kudai baadhi ya malipo yao ambayo hayajakamilika.
Mmoja
wa mawinga wa Yanga, amesema kuwa kuanzia wiki iliyopita, walianza kuzungumza
na watu wanaowataka kuudai uongozi kila wanachodai.
“Unajua
kwa mfumo wa Yanga, hata kama ninaweza kuwa ninadai kitu, basi nawasiliana na
uongozi na hiki kinamalizwa. Lakini wamekuwa wakipita na kutushauri tudai sasa
kabla ya mechi ya Mo Bejaia,” alisema.
Mwingine
ambaye ni beki alisema amekuwa akipata shida na imefikia watu hao waliosema
wanatokea katika matawi matatu tofauti, wanamuona kuwa ni adui.
“Imefikia
sasa wananiona mimi ni adui, hili si jambo sahihi. Kama ninadai basi nitafanya
hivyo na inashangaza wao kutaka ninayedai nifanye hivyo wakati mimi sioni ni
sawa.
“Unajua
wachezaji wa Yanga kaka wamebadilika. Wanajua nini cha kufanya, kwa kifupi
tumeamua kusema wajue, wasituingize kwenye mgogoro tafadhali,” alisema.
Wachezaji wengine walioungana na hao wawili,
wamesisitiza wanataka kuifanya kazi yao kwa ufasaha na wasingependa kuhusishwa
kwenye migogoro.
“Kama kuna tofauti zao za kiuongozi, basi
wazimalizie huko. Nafikiri wanataka kututumia sisi, tufanye vibaya wapate
wanachotaka, si sahihi hata kidogo.”
Championi Jumamosi lilimpata Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka
Deusdedit naye akasema uongozi wao unajua kila kitu.
“Hakuna
tusichokijua, nafikiri kikubwa watu waonyeshe Yanga ni yao na kuacha
kutengeneza matatizo,” alisema na kusisitiza hana muda kwa kuwa wana maandalizi
ya mkutano wa dharura wa wanachama unaofanyika leo kwenye Ukumbi wa Diamond
Jubilee jijini Dar es Salaam.


Post a Comment