MTIHANI wa kwanza wa Kocha Jose
Mourinho wa Manchester United kutwaa taji lake la kwanza klabuni hapo ni kesho
Jumapili wakati timu yake itakapocheza mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya
Leicester City.
Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa
Wembley jijini London ukiwakutanisha bingwa wa Ligi Kuu England ambaye ni
Leicester City na bingwa wa Kombe la FA, Man United.
Mambo mawili yanatazamwa katika
mchezo huu, kwanza ni nguvu ya Leicester City katika kuendeleza ubabe wake kwa
vigogo pia uwezo wa Mourinho katika soka la England akiwa na Man United.
Msimu uliopita wa Ligi Kuu England,
Mourinho aliifundisha Chelsea na hakupata mafanikio kwani aliishia kufukuzwa
wakati Kocha wa Leicester City, Claudio Ranieri alitwaa ubingwa.
Gumzo la mechi hii ni kuona Mourinho
anavyorejea katika soka la England baada ya kuchemka msimu uliopita huku kukiwa
na hatari ya kutolewa nishai na Ranieri raia wa Italia.
MAN UNITED FAIDA, HASARA LEICESTER
CITY
Wakati usajili ukiendelea, inaonekana
Man United ipo katika faida kwa kuwasajili nyota kama straika Zlatan
Ibrahimovic, kiungo Henrikh Mkhitaryan na beki Eric Bailly huku kiungo Paul
Pogba akiwa njiani kusajiliwa muda wowote.
Licha ya kwanza, Mourinho amewapa
mkono wa kuondoka nyota kadhaa wakiwemo
Bastian Schweinsteiger, Adnan Januzaj na wengineo, bado Man United inaonekana
ipo imara.
Yenyewe Leicester City imemuuza
kiungo wake N'Golo Kante kwenda Chelsea lakini imewasajili kipa Ron-Robert
Zieler kutoka Hannover 96 ya Ujerumani, beki Luis Hernández (Sporting Gijon,
Hispania), kiungo Nampalys Mendy (Nice, Ufaransa) na mshambuliaji Ahmed Musa
raia wa Nigeria kutoka CSKA Moscow ya Urusi.
Wachambuzi wa mambo wanaona ni kama
Man United imepata faida ya kuwasajili kina Ibrahimovic kwani wamefiti moja kwa
moja kikosi cha kwanza na kufanya vizuri lakini kuondoka kwa Kante kikosini
Leicester City imeonekana kama tatizo.
NGUVU YA POGBA
Man United hadi sasa ipo katika hatua
za mwisho kumsajili Paul Pogba kutoka Juventus ya Italia na tayari Mourinho
amesema anataka kiungo huyo acheze mechi ya kesho.
Mourinho alitoa kauli hiyo mapema
wiki hii akionyesha kuwa harakati za kumnasa Pogba zipo katika hatua nzuri na
anaamini mchezaji huyo atakuwa msaada mkubwa kwake.
NGUVU YA LEICESTER CITY
Kama ilivyokuwa katika ligi kuu,
nguvu ya Leicester City ipo katika umoja wa kucheza kwa kujituma bila ya
kumtegemea mchezaji muhimu na Ranieri bado ana moyo uleule kwamba hawana la
kupoteza.
“Tunaingia kucheza na timu yenye kila
kitu, sisi kama ilivyo katika ligi kuu hatuna la kupoteza tutacheza kwa nidhamu
ili tushinde,” anasema Ranieri.
MATAJI
Man United inacheza mechi hii ya Ngao
ya Jamii ikiwa imewahi kutwaa ubingwa wake mara 20 huku mara ya mwisho kufanya
hivyo ikiwa 2013, wakati Leicester City imetwaa ubingwa wake mara moja tu na
mara ya mwisho ikiwa 1971.
Leicester City imecheza fainali za
Ngao ya Jamii mara moja tu wakati Man United yenyewe ikiwa imecheza hatua hiyo
mara 29. Katika ligi kuu, Man United imetwaa ubingwa mara 13 wakati Leicester
City imefanya hivyo mara moja tu.
MAN UNITED WABABE
Katika mechi tano walizokutana Man
United na Leicester City kati ya Aprili 13, 2004 na Mei Mosi, mwaka huu, Man
United wameonekana kuwa wababe wakishinda mara mbili huku Leicester City
wakishinda moja na kutoka sare mbili.
Katika mechi hizo, Man United
imefunga mabao tisa huku Leicester City ikifunga manane hivyo kuwa na tofauti
ya bao moja tu.
MAN UNITED ILIPIGWA KIPIGO KIKALI
Septemba 21, 2014 katika mchezo wa
ligi kuu, Leicester City ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa King Power iliifunga Man
United mabao 5-3 na kushangaza wengi.
Katika mchezo huo, mabao ya Leicester
City yalifungwa na Leonardo Ulloa (dk 17 na 83), David Nugent (dk 62 penalti),
Esteban Cambiasso (dk 64) na Jamie Vardy aliyefunga dakika ya 79. Mabao ya Man
United yalifungwa na Robin van Persie dakika ya 13, Angle di María (dk 16) na
Andre Herrera dakika ya 57.
MECHI TANO ZA MWISHO
Katika mechi tano za mwisho ambazo
klabu hizo zimecheza hivi karibuni, Man United imeshinda nne na kufungwa moja
huku Leicester City ikishinda mbili tu ikatoka sare mbili na kufungwa mara
moja.
Kwenye michezo hiyo, Man United
imefunga mabao 13 na kufungwa mabao manane huku Leicester City ikifunga mabao
sita na kufungwa mabao saba.





Post a Comment