IMEDHAMIRIA kufanya kweli msimu ujao kwani timu ya Simba tayari imeonekana kuwa hatari zaidi kwenye safu yake ya ushambuliaji pamoja na ulinzi.
Hali hiyo imekuja baada ya kucheza mechi tatu za kirafiki na kufunga jumla ya mabao 13 huku yenyewe ikiwa haijaruhusu wavu wake kutikiswa hata mara moja.
Katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Polisi Moro, kikosi hicho kinachonolewa na makocha wa kigeni, Joseph Omog kutoka Cameroon na Mganda, Jackson Mayanja, kiliibuka na ushindi wa mabao 6-0 yaliyofungwa na Muivory Coast, Fredric Blagnon na Ibrahim Ajib ambao kila mmoja alifunga mawili, pamoja na Abdi Banda na Mohammed Mussa 'Kijiko' waliofunga kila mmoja moja.
Katika mchezo wa pili dhidi ya Moro Kids, Simba ikaibuka tena na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Ajib na Danny Lyanga.

Katika mchezo wa tatu dhidi ya Burkinafaso, Simba ikashinda tena 5-0, mabao mawili ya Ajib, huku mengine yakifungwa na Moussa Ndusha, Shiza Kichuya na Said Ndemla waliofunga moja moja.
Hiyo inadhihirisha kwamba, Simba imejipanga kikamilifu katika kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kombe la FA kwa msimu ujao.
Omog alisema: “Mabadiliko nayaona kila siku na hii inanipa wakati mzuri wa kujua wachezaji wananielewa kwa kiasi gani.
 “Kikubwa siangalii tunashinda mabao mangapi kwenye mechi za kirafiki, bali ninachoangalia ni vipi wachezaji wanacheza kwa jinsi nilivyowafundisha, hata tukifungwa lakini wamecheza ninavyotaka, basi sitakuwa na shida.”

Post a Comment

 
Top