BAADA ya mfanyabiashara, Mohammed Dewji kutangaza kutaka
kununua hisa nyingi za klabu ya Simba, mashabiki wa timu hiyo sasa wanatembea
kifua mbele na kuanza kuwatupia vijembe wale wote waliokuwa wakiwabeza kutokana
na klabu hiyo kutokuwa na fedha nyingi hapo awali.
Hivi karibuni uongozi uliopo madarakani chini ya Rais Evans
Aveva, ulikubaliana na wanachama wa klabu hiyo kubadili mfumo wa uendeshaji wa
klabu hiyo ambapo katika mabadiliko hayo imetoa nguvu kwa Dewji kufanikisha
azma yake ya kununua hisa nyingi klabuni hapo.
Kutokana na hilo, juzi Jumatano wakati Simba inajiandaa
kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Highlands mkoani
Morogoro, mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakiwapokea wachezaji huku wakilitaja
jina la beki wao wa zamani, Hassan Kessy ambaye amehamia Yanga.
Championi Ijumaa liliwasikia mashabiki hao wakisema Kessy
amepishana na fedha za MO na atajuta kule alipoenda alipodhani ndiyo kutakuwa
na fedha milele.
Mashabiki hao walienda mbali zaidi na kusema watamfanyia kitu
mbaya wakikutana naye mtaani kwani kama inavyojulikana kwamba Kessy ni mzaliwa
wa mkoani Morogoro na familia yake ipo mkoani humo (Gazeti la Championi
haliungi hoja msimamo wao huo kwa kuwa michezo ni furaha na siyo vita).
Ikumbukwe baada ya Simba kukubali kufanya mabadiliko hayo,
tayari Dewji ameshawakabidhi shilingi milioni 100 kwa ajili ya usajili wa
wachezaji ambao watakuja kuunda kikosi bora cha Simba.
Post a Comment