NAHODHA wa Simba, Mussa Mgosi amefunguka kuwa, klabu yao
inapoelekea kusherehekea kutimiza miaka 80, hiyo ni ishara tosha kwamba
inazaliwa upya, hivyo wapinzani wao wakae mkao wa kuumia kila msimu.
Jumatatu ijayo Simba inatarajiwa kusherehekea kutimiza miaka
80 tangu kuanzishwa kwake ambapo sherehe hizo zitafanyika kwenye Tamasha la
Simba Day ambapo kikosi hicho kitacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya FC Leopards
ya Kenya.
Simba ipo kwenye maandalizi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu
Bara unaotarajiwa kuanza Agosti 20, mwaka huu, ambapo kwenye maandalizi yao
ilipiga kambi mkoani Morogoro na kucheza mechi nne za kirafiki na jana Alhamisi
kikosi hicho kilitarajiwa kurejea jijini Dar.
“Kambi tumemaliza salama na naamini mwalimu amekiona kikosi
chake kimeiva. Nisema tu huu mchezo wa mwisho ambao tumefungwa bao 1-0 dhidi ya
KMC ni kipimo tosha kwetu kwani zile mechi za awali tulikuwa kama tunawaonea,
walikuwa hawatoi upinzani wa kweli na hawa jamaa kweli wametupima na tumeona
wapi kuna upungufu.
“Niwaombe mashabiki wa Simba wakae mkao wa kupokea mataji
kwani Jumatatu ijayo klabu yetu hii inazaliwa upya, hivyo baada ya hapo timu
nayo itakuwa mpya na tutaanza kuchukua mataji moja baada ya lingine,” alisema
Mgosi.
Post a Comment