KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog,
amewataka mabosi wa timu hiyo kumpa mkataba mchezaji wa kimataifa, Method
Mwanjali, raia wa Zimbabwe, kufuatia kukikubali kiwango chake huku akiwa anaendelea
kujiridhisha kwa wengine.
Mwanjali ni miongoni mwa wachezaji kadhaa
waliotua Simba kufanya majaribio kwa ajili ya kusajiliwa, wengine baadhi ni Blagnon
Fredrick wa Ivory Coast, Mussa Ndusha na Janvier Besela Bukungu wote wa Congo.
Bosi mmoja ndani ya Kamati ya Utendaji ya Simba
ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema Mwanjali ndiye aliyependekezwa na kocha
hadi sasa huku kocha msaidizi Jackson Mayanja akilipendekeza jina la Bokungu
pia ili waweze kusajiliwa.
“Mwalimu amewakubali Mzimbabwe (Mwanjali) na Bokungu
amependekezwa na Mayanja ambaye anahitaji mchezaji huyo apewe mkataba lakini
kocha anaendelea kuwaangalia pamoja na wachezaji wengine.
“Kocha anahitaji kufanya usajili makini na si wa
kukurupuka, ndiyo maana anatumia muda mwingi kuweza kutoa maamuzi ya nani
asajiliwe kwani anaogopa kumpa mkataba mchezaji ambaye mwisho wa siku atakuwa
mzigo kwenye timu.
“Kocha anaonekana kuwa na msimamo wa hali ya juu
kwa kuhakikisha anatengeneza kikosi imara kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu
ili timu iweze kuwa na ushindani wa hali ya juu ili kuweza kutwaa ubingwa,”
alisema bosi huyo.
Alipopigiwa
simu Omog, alisema majibu yote ya wachezaji watakaosajiliwa yatapatikana
keshokutwa Jumatano.
“Tuna
mechi mbili za kirafiki, Jumatatu (leo) na Jumatano, baada ya hapo ndiyo
nitajua nani wa kumbakisha na nani nimuache, lakini pia hiyo itategemea na
idadi ya wachezaji wa kimataifa inayohitajika kisheria.
“Kama
hawa waliopo wanatimiza idadi ya wachezaji saba basi wote watabaki, kama ikiwa
kinyume nitafanya maamuzi magumu kwa yeyote yule, lakini kwa hivi sasa nawaona
wote wana nafasi ya kuwepo kwa jinsi nilivyowaona,” alisema Omog.
Simba
leo itavaana na Burkina Faso katika mchezo mwingine wa kirafiki, baada ya awali
kuifunga Polisi Moro mabao 6-0, kabla ya kuinyuka Moro Kids 2-0.
Post a Comment