KAMATI
ya Usajili ya Simba, imemtengea kocha wake Mcameroon, Joseph Omog, Sh milioni
350 kwa ajili ya usajili wa wachezaji wapya.
Timu
hiyo iliyoweka kambi yake ya pamoja mkoani Morogoro, tayari imewasajili
wachezaji watano pekee wazawa ambao ni Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim, Hamad
Juma, Mzamiru Yassin, Jamal Mnyate huku ikimchukua Mwadini Ally kwa mkopo
kutoka Azam FC.
Wakati
wakiendelea na maandalizi hayo ya msimu mpya, kocha huyo anaendelea na mchujo
wa wachezaji wa kimataifa kabla ya kuwasajili kwenye msimu ujao.
Akizungumza
kwenye Mkutano Mkuu wa Simba uliofanyika katika Bwalo la Polisi, Masaki jijini
Dar jana Jumapili, Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema kikubwa wanataka kuona
wanakuwa na kikosi imara kitakachopambana na kuchukua ubingwa wa ligi kuu, hayo
ndiyo malengo yao.
Aveva
alisema, katika msimu uliopita timu yao ilishindwa kufikia baadhi ya malengo
ikiwemo la ubingwa kutokana na usajili mbovu walioufanya kwa kusajili wachezaji
wasiokuwa na vigezo vya kuichezea Simba.
Aliongeza kuwa, zoezi hilo la usajili hivi sasa
wamemkabidhi Omog kwa kusaidiana na msaidizi wake Mganga, Jackson Mayanja
kufanikisha usajili huo.
"Uongozi
umetenga bajeti ya shilingi milioni 350 kwa ajili ya kusajili. Na jukumu hilo
la usajili tumemuachia kocha wetu Omog kuhakikisha anakuwa na kikosi bora na
imara kitakachopambana kutwaa taji la ubingwa.
“Hayo
ndiyo malengo tunayotaka kuyatekeleza msimu ujao, ni kupambana kufa au kupona
kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu,” alisema Aveva.
Katika
hatua nyingine, Simba wamepokea nyasi zao bandia ambazo tayari zipo bandarini
tayari kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wao uliopo Bunju jijini Dar.
Aveva
alisema mara baada ya nyasi hizo kufika, uongozi wake upo kwenye hatua ya
mwisho kwa ajili ya kuzitoa bandarini hapo.
Aveva
alisema, mchakato huo wa ujenzi unatarajia kuanza haraka huku akitaja bajeti
nzima ya ujenzi wa uwanja ikiwemo kuweka nyasi bandia kuwa ni Sh milioni 200.
Aliongeza
kuwa, pia uongozi wao umepanga kutengeneza hostel za wachezaji wao
zitakazokuwepo uwanjani hapo kwa thamani ya Sh bilioni 3.4.
Post a Comment