Ikiwa ni siku moja tu baada ya
wanachama wa klabu ya Simba kuridhia mabadiliko ya klabu yao kutoka kwenye
mfumo wa sasa wa uanachama hadi kuwa kampuni ambayo itaendeshwa kibiashara,
bilionea Mohamed Dewji leo amekutana na waandishi wa habari na kusisitiza
kwamba yuko tayari kuweka kitita cha bilioni 20 kwenye klabu hiyo ili amiliki
51% za hisa.
MO amewashukuru wanachama wa klabu ya
Simba kwa kukubaliana kwa pamoja kuunga mkono mabadiliko ya kiuendeshaji kutoka
mfumo wa uanachama kwenda mfumo wa kibiashara na kusema: “Ni lazima tuwafikirie
wanachama kwasababu walitoa damu na jasho lao kwasababu timu yetu ya Simba
kwahiyo ni lazima na wao wanufaike na huu mfumo mpya wa uendeshaji wa
kibiashara.”
Afafanua hoja ya kutofikisha ofa kwa
maandishi
“Viongozi wa Simba wanasema natangaza
kwenye vyombo vya habari dhamira ya kuwekeza kwenye timu lakini sijawahi
kuandika barua kwa uongozi kuhusu dhamira yangu ya uwekezaji kwenye klabu.”
“Nimeshakutana mara kadhaa na
viongozi wa klabu hiyo, nimekutana na Rais wa Simba si chini ya mara tatu,
wameshawahi kuja ofisini kwangu si chini ya mara tatu pamoja na wajumbe wa
kamati ya utendaji na kujadiliana juu ya suala hili.”
“Sisi tulikuwa tunasubiri wanachama
wa Simba waridhie mabadiliko ya mfumo, kwa kuwa wamesharidhia, leo asubuhi
nimetuma barua kwa rais wa Simba kuwaambia niko tayari kuwekeza bilioni 20 kama
watakubali kunipa 51% ya hisa na kufafanua namna ya pesa hizo zitakavyotumika
ndani ya klabu.”
“Barua tayari ameshapata, sasa
namuomba Evans Aveva tuweze kukaa pamoja na kamati ya utendaji na wataalam
wangu kuona uwezekano wa kufanikisha hili jambo haraka iwezekanavyo.
Aahidi kupiga tafu usajili
“Simba ikiridhia kubadili mfumo mimi
nitakuwa tayari kusaidia kwenye usajili, mimi siyo mtu muongo ahadi yangu ipo
palepale nitachangia kwenye mfuko wao wa usajili lakini lazima wao viongozi
waridhie. Kama wao wakinifuata na kuniambia tuko tayari, mimi niko trayari
kuwapiga jeki.”
“Nawashukuru sana wanachama wa Simba,
nawaahidi nitawapigania mpaka na wao wapate hisa kwenye klabu na tutashirikiana
bega kwa bega kuimarisha Simba.
Tayari uongozi wa Simba
umeshamuandikia MO barua ya kuhudhuria kikao pamoja na kamati ya utendaji siku
ya Jumatatu August 15, 2016.
Post a Comment