SIMBA
sasa imekamilika. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya mshambuliaji wake
mpya raia wa Burundi, Laudit Mavugo kuonyesha vitu adimu katika mazoezi ya timu
hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar es Salaam kwa muda
wa dakika 120.
Mavugo alitua nchini juzi Alhamisi akitokea Burundi
ambako alikuwa akiitumikia timu ya Vital’O inayoshiriki ligi kuu ya nchi hiyo
na amekuwa mfungaji bora mara mbili mfululizo ambapo msimu wa 2014/15 alifunga
mabao 32 wakati msimu uliopita wa 2015/16 alifunga mabao 30.
Katika mazoezi hayo ambayo yalikuwa ni ya kwanza kwake
akiwa na kikosi cha Simba lakini pia kwa timu kufanya jijini Dar es Salaam
tangu ilipotoka kambini Morogoro, Mavugo alionyesha kuwa si mchezaji wa
kubahatisha kutokana na uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga pasi,
kukimbia na mpira lakini pia kupiga chenga.
Beki wa kulia wa timu hiyo, Hamad Juma na straika
Frederic Blagnon kwa wakati tofauti walikumbana na balaa kutoka kwa
mshambuliaji huyo baada ya kupigwa chenga za hatari jambo lililosababisha watu
wote waliokuwa uwanjani hapo wampigie makofi Mrundi huyo.
Hali hiyo, pia
ilimpagawisha kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog ambaye alimuita
msaidizi wake, Mganda, Jackson Mayanja kisha wakaanza kujadiliana wakati
mazoezi yakiendelea.
Hata hivyo, baada ya mazoezi hayo, Omog aliliambia Championi Jumamosi: “Namshukuru Mungu
kikosi changu hivi sasa kipo vizuri na tunaendelea na mazoezi yetu kama
kawaida, hata hivyo leo hii nimepata mshambuliaji mpya kutoka Burundi na kazi
yake nimeipenda.
“Kwa siku ya kwanza tu ameonyesha uwezo hivyo ni
matumaini yangu kuwa kadiri siku zinavyoenda basi anaweza kuwa msaada mkubwa
kwetu ila nitamfuatilia zaidi katika mazoezi ya kesho (leo).”
Mavugo ametua Simba akiwa tayari ameshasaini mkataba wa
awali, hivyo jana au leo Jumamosi anatarajiwa kuingia mkataba rasmi wa
kuitumikia klabu hiyo.
Ukiachana na Omog, mashabiki wa timu hiyo pia nao
walimsifia Mavugo ambaye walikuwa wakimsubiri kwa hamu kubwa ajiunge na timu
hiyo tangu msimu uliopita lakini ikashindikana.
Mashabiki hao walimfuata na kumwambia kuwa kazi yake
wameikubali hivyo watahakikisha wanashirikiana naye kwa kumuunga mkono ili
kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri msimu ujao.
“Wachezaji kama huyu ndio tunaotaka, anakuja siku moja
na anaonyesha uwezo, hakika safari hii watatukoma kwani kikosi kimekamilika,
Mavugo piga kazi tupo nyuma yako,” alisikia akisema maneno hayo mmoja kati wa
mashabiki wa Simba waliokuwa uwanjani hapo.
Mavugo alisema: “Nimekuja Simba kufanya kazi na siyo
kutembea, hivyo nitahakikisha natumia nguvu zangu zote ili tuweze kuibuka
mabingwa.
“Najua kuwa timu hii haijachukua ubingwa kwa muda mrefu
lakini kwa jinsi kikosi nilivyokiona kwa haraka hakika sioni kama kutakuwa na
timu ya kutuzuia, hata hao Yanga ambao ni mabingwa hawana wachezaji wenye
vipaji kama hawa niliowaona hapa.”
Aliongeza: “Kama
Amissi Tambwe amekuwa akifunga mabao mengi kwa nini mimi nisifunge?
Nawaambia Wanasimba kuwa Mungu akinijalia uzima, natarajia kufunga zaidi ya
mabao 30 kama nilivyokuwa Burundi, hivyo naomba ushirikiano wao tu wa kutuunga
mkono tunapokuwa uwanjani, kwani wao ni wachezaji wa 12.”
Post a Comment