UNAWEZA kusema leo ni siku ya
neema Yanga, kinachotakiwa ni wanachama kupitisha mabadiliko, klabu iwe kampuni
kwa mfumo wa hisa na bilionea yuko tayari kumwaga Sh bilioni 65 kununua hisa
55%.
Tajiri huyo yuko jijini Dar es Salaam, shabiki wa Yanga
na Mkurugenzi Mkuu wa Kundi la Wanachama wa Yanga la G20, Abbas Shentemba,
amesema kama mwenyekiti wao Yusuf Manji yuko tayari, watamuachia kama la, basi
bilionea huyo, atachukua timu.
Manji ameitisha mkutano
wa dharura leo kuzungumza na wanachama wa Yanga na moja ya ajenda ni kufanya
uboreshaji wa katiba ambayo itawapa nafasi wanachama kuamua ni namna gani
wanataka klabu yao iendeshwe.
“Kwanza niseme
nampongeza sana Manji, amejitolea sana na wanachama na mashabiki tunapaswa
kuheshimu hili. Anatoa fedha zake nyingi, wanaohoji vitu vidogo lakini hawahoji
timu inaishi vipi na wachezaji wanapataje mishahara yao nawashangaa.
“Kikubwa watu wajitokeze
kwenye mkutano na kusikiliza. Kwangu ningewasihi kesho wakubali mabadiliko,
Yanga ijiendeshe kikampuni na kuuza hisa. Mimi nina mfanyabiashara anayetaka
kununua hisa kwa dola milioni 30 (takriban Sh bilioni 65).
“Yeye anataka hisa za
Yanga asilimia 55 tu. Zilizobaki zitakuwa za wanachama wengine. Yuko tayari
kujenga uwanja na yuko tayari kuwaachia Yanga majengo yao.
“Ndiyo maana nimesema
hivi, kama Manji atataka kutoa fedha, basi tutamwachia kwa kuwa ni mtu
aliyejitolea sana, lakini kama hawezi, basi huyu tajiri yupo na yuko tayari
kabisa,” alisema Shentemba na kuongeza:
“Hata suala la kujenga
uwanja, mimi naweza kusaidia kuwalipa fidia watu wa eneo la Jangwani, pia eneo
la Kigogo Sambusa.”
Championi: Huyo bilionea yuko wapi, ni nani hasa?
Shentemba: Wanachama wa Yanga wakikubali mabadiliko, nitamtangaza.
Championi: Vipi hautaki kumtangaza wamjue mapema, asije akawa mamluki?
Shentemba: Mimi ni Yanga, namjua ni Yanga, siwezi kukubali kuiuza Yanga kwa
mamluki.
Championi: Labda ni raia wa Tanzania, asili yake?
Shentemba: Ni Mtanzania, asili yake Tanzania.
Kama kweli hili
litapita, yatakuwa ni mapinduzi makubwa kwenye soka nchini kwa kuwa wiki
iliyopita wanachama wa Simba walikubali kupitishwa kwa mabadiliko na
mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu kama Mo akasema wakikubali anataka
kununua hisa asilimia 51 kwa kitita cha Sh bilioni 20.
Kama kweli alichokisema
Shentemba, maana yake mnunuzi wa Yanga atakuwa ametoa mara tatu na ushee
kununua hisa zinazokaribiana na zile ambazo ametangaza kutaka kununua Mohammed
Dewji ‘Mo’ ndani ya Simba.
Suala la mfumo huu ni
moja ya ajenda zitakazojadiliwa kwenye mkutano wa leo utakaofanyika kwenye
Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar lakini pia kuna hofu kwa baadhi ya wajumbe wa
kamati ya utendaji kwamba wanaweza kutupiwa virago hali ambayo imefanya waanze
kuushambulia uongozi wa Yanga wakitaka kujua mambo kadhaa ambayo hawayaelewi.
Hata hivyo, Makamu
Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga naye alizungumza na kuonyesha kushangazwa na
wajumbe wa kamati ya utendaji kuhoji kwenye vyombo vya habari.
“Ninazungumza na kila
mjumbe, wangeweza kuniambia. Tulifanya kikao mimi nilimwakilisha mwenyekiti,
lakini vipi leo tulumbane kwenye vyombo vya habari? Sehemu sahihi ya kusemea
kwa wajumbe wa kamati ya utendaji ambao ni viongozi, wanajua ni wapi,” alisema
Sanga.
Post a Comment