KOCHA wa
Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, ameyachomolea maombi ya kuifundisha timu
ya taifa ya Ghana inayonolewa kwa sasa na Muisrael, Avram Grant, kocha wa
zamani wa Chelsea, West Ham na Portsmouth.
Pluijm alipewa
maombi hayo na kusisitiziwa juu ya suala hilo na Chama cha Soka Ghana (GFA)
alipokwenda na Yanga nchini humo kuivaa timu ya Medeama wiki moja iliyopita
katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Imeelezwa
kwamba Ghana ilimpendekeza Pluijm kuchukua mikoba hiyo baada ya kutoridhishwa
na utendaji kazi wa Grant wa kutotulia nchini humo, zaidi amekuwa akitumia muda
mwingi akiwa Uingereza.
Lakini
taarifa ni kwamba, Pluijm akawaeleza kuwa hataweza kujiunga na kikosi hicho
kilichosheheni mastaa kibao kama Asamoah Gyan anayekipiga Shanghai SIPG nchini
China, Jordan Ayew (Aston Villa), Thomas Partey (Atletico Madrid), Andre Ayew
(Swansea), Christian Atsu (Malaga) na wengine wengi kwa kuwa siku chache
zilizopita aliongeza mkataba wa miaka miwili wa kuinoa Yanga na bado ana
mipango mirefu na timu hiyo.
“Kweli
walinifuata, wakawasilisha ombi lao la kuhitaji niinoe timu ya taifa ya Ghana.
Kwanza niseme ni heshima kubwa kupewa nafasi katika timu kama hiyo lakini
nikawaeleza kwamba ni ngumu kwa kuwa siku chache nyuma nimetoka kusaini mkataba
mpya na Yanga kwa ajili ya mipango mingi ya baadaye.
“Najua
wananifahamu ndiyo maana wamenipa nafasi hiyo lakini kwa sasa ni ngumu, nipo na
Yanga na niseme tu kwamba bado nina mipango zaidi nikiwa hapa,” alisema Pluijm
mwenye kadi ya uanachama wa Yanga yenye makao makuu yake, Kariakoo, Dar es
Salaam.
Pluijm
ambaye makazi yake ni nchini Ghana, kabla ya kutua Yanga aliwahi kuzinoa timu
kadhaa za nchini humo tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000 zikiwemo Heart of Lions,
Ashanti Gold, Medeama, Berekum Chelsea na nyingine.
Kwa misimu
miwili aliyoifundisha Yanga, Pluijm ambaye ni Kocha Bora wa Ligi Kuu Bara msimu
uliopita, amefanikiwa kuipa Yanga ubingwa wa ligi mara mbili, Kombe la FA na
kutinga kwenye hatua ya nane bora ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Post a Comment