WINGA mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Enock Atta Agyei, jioni hii ameifungia Medeama ya Ghana moja ya mabao muhimu katika ushindi wa 3-2 dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo).
Nyota huyo alikuwa sambamba kikosini na beki mwingine aliyesajiliwa na mabingwa hao wa Kombe la Kagame, Daniel Amoah, ambaye anatarajia kutua nchini muda wowote kuanzia sasa mara baada ya kumaliza mchezo huo.
Atta, 17, aliyerejea Medeama katika mchezo huo muhimu wa Kundi A la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika alifunga bao hilo dakika ya 31 kwa mkwaju wa faulo ya moja kwa moja uliompita kipa mkongwe wa Mazembe, Sylvain Gbohouo, kabla ya mechi hiyo kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao hilo.
Moses Sarpong aliiongezea Medeama bao la pili kwa mkwaju wa penalti iliyotokana na Coulibaly Salif kuunawa mpira wakati akijaribu kumzuia Atta Agyei, kabla ya TP Mazembe kusawazisha mabap yote kupitia kwa Jonathan Bolingi Mpangi na Rainfold Kalaba.
Wakati watu wakidhania mchezo huo ungemalizika kwa sare hiyo, Kwasi Donsu aliishangaza TP Mazembe kwenye dakika za nyongeza akifunga bao la tatu la ushindi.
Bao hilo linaifanya Medeama kuhitaji sare yoyote wikiendi ijayo dhidi ya MO Bejaia kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi A, ili iweze kuwazidi kete Waaljeria hao na kusonga kwa hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo wakiifuata TP Mazembe, ambayo tayari imeshafuzu.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kuaga rasmi michuano hiyo na sasa wanasubiria mchezo wa mwisho watakaocheza na TP Mazembe ugenini jijini Lubumbashi.

Post a Comment

 
Top