HATMA ya uongozi wa Simba kumuuzia timu hiyo bilionea, Mohammed Dewji inatarajiwa kujulikana leo Jumatatu mara baada ya kamati husika iliyopewa kusimamia mchakato huo kukutana na tajiri huyo.
Hiyo, ni sehemu ya ahadi ya rais wa timu hiyo, Evans Aveva aliyoitoa kwenye mkutano mkuu uliofanyika mwezi uliopita katika Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Masaki jijini Dar es Salaam baada ya wanachama kupendekeza kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.
Awali, uongozi wa timu hiyo uligoma kubadili mfumo huo wa uendeshaji wa klabu hiyo kutoka kwa wanachama na kuwa kampuni baada ya MO kuomba kuwekeza hisa.
Kwa mujibu wa taarifa ilizozipata Championi Jumatatu, kamati hiyo maalum iliyopewa kusimamia mchakato huo, itakutana kwa mara ya kwanza kujadili mapendekezo ya MO kabla ya kuyapitia kwa pamoja ili kufikia muafaka wa suala hilo mapema.
Mtoa taarifa huyo alisema, hiyo ndiyo ajenda kubwa watakayoijadili katika kikao hicho, kikubwa wanataka kufanya maamuzi sahihi ili hapo baadaye wasiyajutie.
“Kikubwa tutajadiliana masuala hayo na tunataka tufikie muafaka mzuri kabla hatujachukua maamuzi ya kumkabidhi klabu ili baadaye tusije tukayajutia,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa timu hiyo, Patrick Kahemele kuthibitisha hilo alisema: “Hizo taarifa ulizozipata za kamati kukutana na MO ni za kweli kabisa. Tunaamini tutafikia muafaka mzuri na MO, katika kikao hicho kamati husika itapitia maombi na mapendekezo kabla ya kumkabidhi klabu na maamuzi sahihi ni kitu muhimu ili baadaye tusije kujutia."

Post a Comment

 
Top