KOCHA Mkuu wa Azam, Mhispania, Zeben Hernandez,
amesema kikosi chake kipo vizuri katika kila idara, isipokuwa kwenye eneo la
ushambuliaji linaloongozwa na John Bocco ambapo hapo ndipo kunaonyesha upungufu
kutokana na washambuliaji wake kuwa ‘butu’ kwa kushindwa kufunga mabao.
Zeben wikiendi iliyopita alikishuhudia kikosi
chake kikilazimishwa sare ya bao 1-1 na URA ya Uganda katika mchezo uliopigwa
Uwanja wa Chamazi, Dar Ijumaa iliyopita. Mchezo huo ulikuwa wa pili kwa Azam
kutoka sare baada ya kufungana bao 1-1 na Ruvu Shooting ya Pwani.
Katika mechi zake, Azam inaonekana kumkosa
vilivyo straika Kipre Tchetche ambaye aliuzwa nchini Oman.
Zeben amesema kuwa safu yake ya ushambuliaji
ndiyo inayomuumiza kichwa mpaka sasa kutokana na kutokuwa fiti kwa kushindwa
kufunga mabao kwenye nafasi ambazo wanazitengeneza.
“Tupo tayari kwa mapambano ya ligi pamoja na
mchezo wetu ujao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga lakini tuna dosari kidogo
kwenye nafasi ya ushambuliaji ambapo wanahitaji marekebisho kidogo ili kuwa
katika kiwango kile ambacho mimi nakitaka.
“Siyo kwamba ni wabaya kabisa, hilo hapana, ila
wanachokosea ni kutokuwa siriazi kwenye kumalizia nafasi zile ambazo tunakuwa
tunazitengeneza na mechi hizi mbili zilizopita ni ushahidi tosha lakini
nitawapa mazoezi ya kuwafanya kuwa bora zaidi kabla ya kuanza kwa ligi,”
alisema Zeben.
Azam kwa sasa ina washambuliaji John Bocco na
Mzimbabwe, Bruce Kangwa mara baada ya kuachana na washambuliaji wake Didier
Kavumbagu, Allan Wanga (wameachwa) sambamba na Tchetche aliyetimkia timu ya Al
Nahdha.
Post a Comment