MPANGO wa kipa wa Azam FC, Mwadini Ali kutua Simba kwa mkopo
umeingia mchanga baada ya kipa huyo kudaiwa kuweka masharti magumu kuhusu
uhamisho wake huo.
Ilielezwa kuwa ilikuwa imekubaliwa Simba wamchukue Mwadini na
straika mwingine wa Azam FC, Ame Ali lakini mpaka sasa dili lililokamilika ni
la Ame kutua kwa Wekundu hao kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Chanzo makini kutoka Azam kimeeleza kwamba ishu hiyo imeyumba
kwa kuwa Mwadini ametaka apewe dau la usajili ambalo halikuwekwa wazi, ndiyo
atue Simba.
“Tatizo ni kwamba Mwadini hajali kama anakwenda kwa mkopo
Simba, anachokitaka ni dau la usajili, sasa hiyo Simba hawajaafiki ndiyo maana
kumekuwa na ugumu juu ya uhamisho wake.
“Kuna asilimia ndogo za kukamilika kwa ishu hiyo kwa sababu
Simba wanaonekana kuanza mipango mipya ya kutafuta kipa sehemu nyingine,”
kilisema chanzo hicho.
Walipotafutwa Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange
‘Kaburu’ na Katibu Mkuu, Patrick Kahemele kulitolea ufafanuzi suala hilo, wote
wawili hawakupokea simu zao za mkononi.
Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba alipotafutwa alisema:
“Ninachokifahamu ni kwamba mchezaji hasukumwi kwenda kwa mkopo, kuna
makubaliano baina yake pia lakini kwa kuwa Simba ndiyo wamemhitaji mchezaji,
ingekuwa vizuri wao wakatolea ufafanuzi walipofikia.”
Post a Comment