MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji, amevunja ukimya na kusema Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Jerry Muro yupo huru na anaendelea na kazi zote za klabu kama kawaida.
Manji amesema, klabu hiyo haina taarifa yoyote rasmi ya kufungiwa kwa Muro.
“Kama taarifa tumesikia kwenye magazeti na redio, kweli taasisi kama Yanga, msemaji wake anasimamishwa kwa njia hiyo?
“Hao waliomsimamisha pia ni taasisi, vipi wafanye hivyo. Yanga tunawezaje kuamini hilo? Muro bado yuko kazini na anaendelea na shughuli zake kama kawaida,” alisema Manji.
Manji amesisitiza kuwa kama ni kweli basi TFF inapaswa kutoa hukumu ya kumfungia Muro kama ambavyo wamekuwa wakisikia.
TFF kupitia kamati ya nidhamu ilitangaza kumfungia Muro mwaka mmoja ikiwa ni pamoja na kumpiga faini.

Lakini imekuwa ikisita kutoa hukumu yake inayohusiana na Muro, jambo ambalo linaifanya Yanga kuona kuna upotofu wa mambo na kukiukwa kwa usahihi.
Juhudi za gazeti hili kupata hukumu ya Muro zimekuwa zikigonga ukuta hasa kutokana na kuhoji makosa yaliyomtia hatiani na viongozi wa TFF wamekuwa wakisisitiza bado inaandaliwa jambo ambalo haliwezekani kuchukua muda mrefu hivyo.

Post a Comment

 
Top