SIKU chache baada ya Msemaji wa Simba, Haji Manara kukumbwa na ugonjwa wa macho na kulazimika kupatiwa matibabu nchini India, makamu mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ amelazimika kufanyiwa operesheni ya tumbo baada ya kugundulika kuwa na uvimbe.
Mzee Kinesi alishika nyadhifa mbalimbali ndani ya Simba kabla ya kujiweka kando ya mambo ya kiuongozi, mwaka juzi kwa ajili ya kusimamia miradi ikiwemo ukarabati wa uwanja wake wa Kinesi uliopo Shekilango jijini Dar.
Kiongozi huyo aliyewahi kukalia kiti cha mwenyekiti baada ya ‘kupinduliwa’ kwa Ismail Aden Rage mwaka 2013, alisema alikuwa akihisi maumivu makali tumboni kabla ya Jumamosi iliyopita kulazimika kulazwa katika Hospitali ya Muhimbili.
“Nilikuwa nikihisi maumivu makali sana, Jumamosi nilikwenda Muhimbili baada ya uchunguzi niligundulika kulikuwa na uvimbe tumboni, kesho yake nikafanyiwa oparesheni.
“Kwa sasa niko nyumbani baada ya kuruhusiwa Jumanne ya wiki hii, namshukuru Mungu afya yangu inaendelea kuimarika japo bado sijapona,” alisema Kinesi.

Post a Comment

 
Top