WAKATI lile sakata la beki wa Yanga,
Hassan Kessy likiwa bado halijapatiwa ufumbuzi wa kuruhusiwa kucheza katika
klabu yake mpya ya Yanga, jambo jipya limeibuka katika mkataba huo kufuatia
maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kubaini kuchezewa kwa mkataba wake
uliotoka Simba na kulifanya shirikisho hilo liwe na tahadhari katika mikataba
mingine ya wachezaji msimu ujao.
Kessy alitua Yanga kabla ya mkataba
wake na Simba kufikia tamati kufuatia mgogoro uliojitokeza kati ya mchezaji
huyo na uongozi wake, hivyo kuamua kuachana na timu hiyo na kuhamia Yanga, hivi
karibuni.
Kikizungumza na Championi Ijumaa, chanzo kutoka TFF, kimefunguka kuwa mkataba wa
mchezaji huyo ambao umefikishwa TFF kutoka Simba ni tofauti na aliouwasilisha
Kessy.
Aidha, imeelezwa kuwa, kutokana na
hali hiyo iliyojitokeza katika mkataba wa Kessy, imeizindua TFF kuhakikisha
wanakuwa makini na mikataba ya wachezaji watakaosajiliwa msimu huu kuhakikisha
wanaondokana na matatizo kama hayo kwa kuhakikisha kabla ya wachezaji kupewa
mikataba kwanza lazima isainiwe na TFF ili kuhakikiwa kisha ndipo itolewe kwa
pande zote husika.
“Mkataba wa
Kessy umechezewa kwa kiasi kikubwa kwa upande wa Simba wenyewe ambao wameuleta
hapa ukiwa umefutwa baadhi ya vipengele na kwa upande wa mkataba aliouwasilisha
mchezaji na wenyewe una upungufu kufuatia baadhi ya karatasi kutokuwepo, hivyo
ni kiasi gani inaonekana kuna mchezo umechezwa pande zote mbili.
“Hali hiyo imeifanya Yanga kuwa njia panda kwa kutojua
mkataba upi ni sahihi hivyo wanahofia kupatwa matatizo zaidi hapo mbele, pia huenda
mchezaji huyo akashindwa kucheza msimu ujao wa ligi kuu.
“Katika mikataba iliyowasilishwa kuna kipengele kinaonyesha
kuwa Kessy alikubaliana na Simba kuwa asiruhusiwe kwenda kokote hadi pale klabu
yake hiyo itakaporidhia kuondoka, hivyo kwa sasa itakuwa ngumu kucheza Yanga
hadi Simba iridhie kumruhusu kwenda kucheza katika klabu yake hiyo mpya.
“Kutokana na upungufu ambao tumeuona kwenye mkataba wa Kessy
viongozi kwa pamoja wameamua kujiongeza kwa kuhakikisha kila kitu kwa sasa
kinakwenda kwa umakini wa hali ya juu na ndiyo maana yametolewa maamuzi ya
nakala zote za mikataba ya wachezaji kuwasilishwa TFF na kusainiwa kwanza hapa
ofisini kabla ya kwenda kwa klabu na mchezaji.
“Kopi zitakazotakiwa kutolewa ni tano ambapo mara baada ya
kusainiwa moja itabaki TFF nyingine atapewa mchezaji na nakala nyingine
itakwenda kwa klabu na nyingine zitakuwa akiba ili kuondoa mkanganyiko kama
uliojitokeza kwa Kessy ambapo hadi sasa mambo yanaonekana kuwa magumu kwa
kushindwa kupatikana ufumbuzi kwa kutotambua mkataba upi ni sahihi.
“Asilimia ya mchezaji huyo kucheza msimu ujao ni ndogo
iwapo uongozi wake hautakubali kukaa na Simba kufanya mazungumzo kwani Simba
inahitaji kiasi cha shilingi milioni 130 kutokana na kukiuka kanuni kwa kumtumia
mchezaji huyo kabla ya mkataba wake kuisha,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa TFF, Afred Lucas kuzungumzia
suala hilo alisema: “Suala hilo bado halijapatiwa ufumbuzi lakini kuhusu
mkataba wake kuchezewa sina taarifa hizo.”
Post a Comment