ILIKUWA furaha ya aina yake kwa
mashabiki wa Yanga baada ya timu hiyo kukabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu
Tanzania Bara, lakini ilikuwa huzuni kushindwa kuibuka na ushindi dhidi ya
Ndanda FC ya Mtwara na kutoka sare ya mabao 2-2.
Mchezo huo wa raundi ya 29
ulifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo hadi mapumziko Yanga ilikuwa
mbele kwa mabao 2-1.
Ndanda ilikuwa ya kwanza kupata
bao dakika ya 29 mfungaji akiwa Omari Mponda kwa njia ya penalti baada ya
Raphael Amiri kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Thabani Kamusoko.
Hata hivyo dakika sita baadaye
Simon Msuva aliisawazishia Yanga kutokana na pasi ya Geofrey Mwashiuya na
dakika ya 40 Donald Ngoma aliifungia Yanga bao la pili, akimalizia mpira wa
Haji Mwinyi.
Timu hizo zilishambuliana kwa zamu
karibu muda mwingi wa kipindi cha pili, lakini umaliziaji ulikuwa tatizo kwa
kila upande.
Wakati mashabiki wakiamini pengine
mchezo ungemalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi huo, huku furaha ikiongezeka
kwa mashabiki wa klabu hiyo, mambo yalibadilika dakika ya 79 wakati Salum
Minely aliposawazisha bao hilo akimalizia kazi ya Atupele Green na kuwafanya
mashabiki wa Yanga kutulia kwa muda.
Wachezaji wa Yanga walijipanga na
kushambulia kwa nguvu kutaka kuongeza bao la tatu, lakini Ndanda FC ilijipanga
na kuhakikisha mchezo huo unamalizika kwa sare.
Furaha ya mashabiki wa Yanga
ilirejea kwa nguvu zaidi, baada ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu
Nchemba aliyekuwa mgeni rasmi katika mchezo huo kumkabidhi nahodha wa Yanga,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kombe la ubingwa wa ligi hiyo msimu wa 2015/16.
Ni taji la 26 katika historia ya
klabu hiyo kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa ndiyo timu iliyochukua taji hilo
mara nyingi, ikifuatiwa na mpinzani wake wa jadi Simba iliyotwaa ubingwa mara
18.
Yanga imekabidhiwa kombe hilo
mapema kabla ya ligi kumalizika, baada ya katikati ya wiki hii kufikisha pointi
71 ambazo hakuna timu nyingine yoyote inaweza kuzifikia, ambapo kwa matokeo ya
jana imefikisha pointi 72.
Azam FC inashika nafasi ya pili
ikiwa na pointi 60 na ikishinda mechi zake mbili zilizosalia itafikisha pointi
66, wakati Simba yenye pointi 59 ambayo leo inacheza na Mtibwa Sugar Uwanja wa
Manungu, Turiani ina uwezo wa kufikisha pointi 65 ikishinda mechi zake mbili
zilizosalia.
Mechi nyingine za ligi hiyo leo
itakuwa kati Kagera Sugar ya Bukoba itaikaribisha Stand United ya Shinyanga
Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga,
Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Mbeya City.
Prisons itaikaribisha Toto
Africans ya Mwanza Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Uwanja wa Mkwakwani, Tanga
African Sports watakuwa wenyeji wa Azam FC.
Ligi Kuu itamalizika Mei 21, mwaka
huu, ambapo Mbeya City itacheza na Ndanda FC (Mbeya), Coastal Union na Prisons
(Tanga), Simba SC na JKT Ruvu (Dar es Salaam), Toto Africans na Stand United
(Mwanza), Azam FC na Mgambo JKT (Dar es Salaam), Kagera Sugar na Mwadui FC
(Shinyanga), Mtibwa Sugar na African Sports (Morogoro) na Majimaji na Yanga SC
(Songea).
Post a Comment