Ariana Yohana
SAFARI ya kukamilisha mpangilio wa timu nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu ya England ‘Premier League’ unaendelea kuwa mgumu baada ya vigogo wawili katika nafasi hiyo kutoka sare huku timu moja ikipata kichapo.
Baada ya Leicester City kutwaa ubingwa na kukabidhiwa kombe, kazi imebaki katika timu zinazofuata chini ambapo Arsenal na Manchester City zimetoka sare ya mabao 2-2 huku Tottenham Hotspur ikipata kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Southampton, mechi zote hizo zikipigwa jana Jumapili.

Kutokana na matokeo hayo timu zitakazomaliza katika nafasi ya pili, tatu na nne zitajulikana baada ya mechi za mwisho za ligi hiyo zinazotarajiwa kuchezwa wikiendi ijayo.
Man City ndiyo iliyoanza kufungua ukurasa ambapo ilifunga bao katika dakika ya 8 kupitia kwa Sergio Aguero lakini bao hilo halikudumu muda mrefu kwa kuwa dakika mbili baadaye Olivier Giroud aliisawazishia Arsenal na kufanya matokeo kuwa sare mpaka mapumziko.

Mabao ya kiwango cha juu yaliyofungwa na Kevin de Bruyne dakika ya 52 kwa upande wa Man City na lile la dakika ya 68 la Alexis Sanchez yalifanya mchezo huo umalizike kwa sare hiyo.
Hivyo sasa, kutokana na matokeo hayo Tottenham imebaki nafasi ya pili, Arsenal ya tatu na Man City ya nne huku Man United ikiwa nafasi ya tano, matokeo ya mechi za mwisho yanaweza kuchangia mabadiliko ya timu hizo katika nafasi hizo za juu. 

Manchester United inacheza na West Ham kiporo Jumanne hii kwenye Uwanja wa Upton Park, kama ikishinda maana yake itaishusha City hadi nafasi ya tano na yenyewe kusonga hadi nafasi ya nne. Mechi nyingine ya ligi hiyo ilishuhudia Liverpool ikipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Watford wafungaji wakiwa ni Joe Allen dakika ya 35 na Roberto Firmino dakika ya 76. 

Hii inamaana kuwa kama Man City kama haitamaliza Top 4 basi pep Guardiola ambaye atakichukua kikosi hicho mwishoni mwa msimu huu basi atashiriki ligi ndogo ya UEFA maarufu kama EUROPA LEAGUE. 

Post a Comment

 
Top