KOCHA Mkuu mtarajiwa wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na
Kati Azam FC, Zeben Hernandez, ameweka wazi kuwa malengo yake makubwa ni
kuifanya timu hiyo kuwa timu kubwa barani Afrika msimu ujao.
Kocha huyo raia wa Hispania aliyekuwa akiinoa Club Deportivo
Santa Ursula ya Ligi Daraja la Tatu nchini humo, ametua nchini juzi pamoja na
Kocha wa Viungo Jonas Garcia kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa
timu hiyo kabla ya kusaini mkataba wa kuinoa Azam FC msimu ujao.
Makocha hao wametua kufuatia Kocha Mkuu wa sasa wa Azam FC,
Stewart Hall, kutangaza kuachia ngazi mwishoni mwa msimu huu kufuatia
kutoridhishwa na matokeo ya hivi karibuni ya timu hiyo.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz leo
asubuhi mara baada ya kuwasili mkoani Tanga kushuhudia mchezo wa timu hiyo
dhidi ya African Sports jioni ya leo, Hernandez amewaambia mashabiki wa Azam FC
kuwa watarajie ubora wa timu msimu ujao utakaoifanya kuwa timu bora Afrika.
“Ninafuraha kubwa, Azam itakuwa timu bora msimu ujao,
tutafanya kazi kwa bidii kila mara na kuifanya Azam kuwa timu kubwa Afrika,”
alisema.
Aifurahia Tanzania
Hernandez hakusita kuelezea furaha yake kutokana na watu
aliokutana nao Tanzania, ambapo amesema kuwa: “Ninafuraha kubwa, watu wa hapa
ni wazuri na waliojipanga, na mpira wa hapa una vipaji vingi, wachezaji wengi
kuwa na vipaji ni jambo muhimu kwa mpira wa Tanzania, Tanzania kama nchi ni
sehemu nzuri sana na ninafuraha sana kwa hilo.”
Ujio wao ndani ya Azam FC
“Malengo yetu ni kuifanya Azam kuwa na mfumo mpya wa soka la
kisasa kuanzia utambulisho kama timu, mbinu zetu za kufanya kazi na pia katika
mechi…Kwangu mimi na mwenzangu kufanya kazi Afrika ni uzoefu mzuri na
tunafuraha sana,” alisema.
Kwa upande wake Jonas Garcia aliyeambatana naye alionyesha
furaha kubwa kuja Azam FC huku akisema kuwa watafanya kazi kwa bidii sana kwa
ajili ya kuipa ubora timu hiyo.
C.E.O afafanua ujio wao
Akizungumzia ujio wa makocha hao, Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Azam FC, Saad Kawemba, amesema kuwa mara baada ya kuwasili juzi tayari wameanza
nao mazungumzo jana kwa ajili ya kukinoa kikosi hicho msimu ujao.
“Tumewapokea juzi Dar es Salaam tunamshukuru Mungu, jana
tulikuwa nao na tumeanza mazungumzo, leo wako hapa Tanga kuangalia mchezo
(African Sports vs Azam FC) na watafanya tathimini yao, kwa hiyo mazungumzo
bado yanaendelea na katika hali ya kawaida tukifanikiwa kwa maana yake watakuwa
wanachukua timu yetu ya Azam kwa msimu unaokuja, jambo jema kwetu ni kwamba
makocha hao bado ni vijana na wanadhamira ya kupata mafanikio, hivyo hiko ni
kitu ambacho tunajivunia.
“Lakini bado tunasema kwamba bado tunazungumza nao
hatujafika nao muafaka mpaka mwisho, lakini tunachopenda kusema ni kwamba
tunawaomba mashabiki wetu wawe watulivu timu ipo na kocha bado yupo (Stewart
Hall) na anamalizia muda wake na kuhakikisha ya kuwa kila kitu kinakwenda
sawasawa kabla ya msimu haujaisha,” alisema.
Bosi huyo aliyebobea kwenye mambo ya uongozi wa soka na
kutambulika na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Duniani (FIFA), alimalizia
kwa kusema kuwa wanatarajia kufanya mkutano na waandishi wa habari kesho
Jumatatu mara baada ya kumalizia mazungumzo ya mwisho na makocha hao, ambapo
ataweka wazi kila kitu kuhusu muundo wa benchi la ufundi msimu ujao.
Post a Comment