Hakuna kulala leo FA Cup na Copa del Rey
KOCHA wa Manchester United, Louis van Gaal leo anajaribu kutwaa taji lake la kwanza akiwa na klabu hiyo katika fainali ya Kombe la FA dhidi ya Crystal Place kwenye Uwanja wa Wembley.
Hii ni fainali ya 19 kwa Man United katika Kombe la FA ikiwa inasaka rekodi ya Arsenal ambayo imetwaa taji hilo mara 21 huku timu hiyo ya Van Gaal ikiwa imelibeba mara 11.
Kuelekea mchezo huo, Van Gaal amesema anaamini mashabiki wa Man United wanawaza zaidi kutwaa ubingwa kuliko majaliwa ya ajira yake klabuni huku Kocha Jose Mourinho akitajwa kuchukua nafasi yake.
"Nafikiri mashabiki wana hamu ya kuona klabu ikitwaa mataji kuliko kusikia habari zangu. Tunataka tuwape wanachotaka, hapa nafanya kazi na wachezaji 27, wote hao wanataka tufanikiwe,” alisema Van Gaal raia wa Uholanzi.
Man United iliyomaliza Ligi Kuu England katika nafasi ya tano, itamtegemea zaidi nahodha Wayne Rooney na mshambuliaji kinda Marcus Rashford.
Kwa upande wake, Kocha wa Crystal Palace, Alan Pardew, alisema anaamini kikosi chake kitafanya vizuri katika mchezo huo utakaochezeshwa na mwamuzi Mark Clattenburg kwani hakina presha kama ilivyo kwa Man United.
"Nafikiri presha zaidi ipo kwao, wao ni timu kubwa kuliko sisi hivyo tuna nafasi ya kufanya vizuri. Najua wapinzani wana matarajio makubwa lakini wachezaji wangu nao wanaona huu ni wakati wao,” alisema Pardew.
Kikosini mwake, Pardew atawategemea zaidi Emmanuel Adebayor, Wilfried Zaha na Yohan Cabaye ambao wanaonekana kuelewana kwa sasa.
Katika nusu fainali, Man United iliitoa Everton huku Crystal Palace ikiitoa Watford.
Wakati huohuo, kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Vicente Calderon jijini Madrid, Hispania unaoingiza mashabiki 54,907, Barcelona itacheza fainali ya Copa del Rey dhidi ya Sevilla.
Hadi kufika hatua hiyo, Barcelona ambayo pia ni bingwa mtetezi iliifunga Valencia katika nusu fainali huku Sevilla ikiifunga Celta Vigo kwenye hatua hiyo.
Tayari figisu zimeanza kuonekana kabla ya fainali hiyo baada ya mamlaka za Jiji la Madrid, kukataza bendera ya Catalan kupeperushwa katika mechi hiyo. Barcelona inayotokea Catalan ndiyo inayoongoza kutwaa taji hilo ikiwa imelibeba mara 27.
Post a Comment