MANUEL PELLEGRINI amemuonya kocha anayekuja kuchukua nafasi yake Manchester City, Pep Guardiola kwamba Ligi Kuu England kamwe haitaweza kumsamehe.
Pellegrini ataiongoza Man City katika mchezo wa mwisho utakaofanyika Jumapili  dhidi ya Swansea na Guardiola ataanza kazi rasmi Julai Mosi.
Kocha Guardiola ameshinda Ligi ya Mabingwa mara mbili na Ligi ya Hispania mara tatu alipokuwa na kikosi cha Barcelona, na anaondoka Bayern Munich mwishoni mwa msimu akiwa ameshinda Ligi ya Bundesliga mara tatu mfululizo.
Lakini Pellegrini amemuonya Guardiola kutokana na ukali wa Ligi Kuu England na anaweza kupata mshtuko wa utamaduni, pamoja na kwamba na kwamba ni mmoja kati ya makocha bora duniani.
“Bila shaka inakuwa ni changamoto mpya kama inakuwa ni mara yako ya kwanza kushiriki Ligi Kuu England,”alisema Pellegrini.
“Simzungumzii Guardiola, ninajizungumzia pia miye mwenyewe mara yangu ya kwanza nilipowasili hapa.
“Lakini pindi unapokuwa umefanya kazi Ulaya kwa miaka mingi kama kocha, unajiandaa kukubaliana na changamoto.
“Nina uhakika na hilo, kuwapo kwenye ligi ngumu, Guardiola anatakiwa kujiandaa kufanya hivyo.
“Unajiandaa kwa muda wako wote. Unacheza katika Ligi ya Mabingwa dhidi ya timu za Kiingerezana kuiangalia Ligi ya Kiingereza kila wiki.
“Bila shaka si sawa na wanaoshi kila wiki hapa kwa ajili ya Ligi Kuu, lakini kila kocha mzuri amejiandaa kwa hilo.
“Nadhani (Ligi Kuu) itakuwa na ushindani zaidi kwa sababu kila msimu haki za maonesho ya TV zinapanda bei, kwa hiyo kila timu itakuwa na pesa ya kutosha kununua wachezaji wazuri.
“Kila timu ya Ligi Kuu ina wachezaji wazuri, lakini labda kwa zile kubwa kuna tofauti kidogo.
“Timu kubwa zinazocheza mashindano ya Ulaya zina changamoto mbili-kufanikiwa katika ligi ya ndani na ile ya Ulaya.”
Kazi kubwa ya mwisho ya Pellegrini kama bosi wa Man City ni kuhakikisha anapata sare au anashinda dhidi ya Swansea Jumapili kumhakikishia Guardiola heshima ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Lakini hata kama Man City itajihakikishia kwa Ligi ya Mabingwa, Pellegrini amemwambia Guardiola itakuwa ni vigumu kuweza kupata mafanikio katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa.
“Sababu kwa nini hatukuweza kushinda Ligi Kuu, kwanza Leicester ilikuwa ni timu nzuri na ilicheza vizuri, na la pili kwa sababu tulicheza michezo mingi zaidi,” alisema Pellegrini.
“Sababu ya tatu ni kwa sababu tuliendelea katika Ligi ya Mabingwa hadi nusu fainali na tukiwa na mtihani dhidi ya Manchester United, Arsenal na Tottenham.
“Kwa hiyo ni vigumu kufikia nafasi ya kwanza hadi ya nne na  hiyo ni kwa nini itakuwa ni vigumu kwa miaka kadhaa kuweza kufikia Top Four.”

Post a Comment

 
Top