LEICESTER City imeanza maandalizi yake ya kuelekea kwenye
michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kutaka kuwaongezea mikataba kocha wa
timu hiyo, Claudio Ranieri na kiungo wao mshambuliaji, Riyad Mahrez.
Imeelezwa kuwa katika mkataba huo mpya Ranieri anatarajiwa
kulipwa pauni milioni 3 kwa mwaka ikiwa ni mara mbili ya mshahara wake wa sasa.
Upande wa Mahrez ambaye alipata Tuzo ya Mchezaji Bora wa
Mwaka (PFA) anatarajiwa kulipwa pauni 75,000 kwa wiki kiwango ambacho
kitamfanya awe mchezaji anayelipwa zaidi klabuni hapo akiwa sawa na Jamie
Vardy.
Makubaliano ya pande mbili baina ya klabu na wahusika hao
yanatarajiwa kuanza wiki chache zijazo mara baada ya msimu huu kumalizika.
Inadaiwa kuwa Mahrez yupo tayari kuongeza mkataba kwa kuwa
timu hiyo itashiriki katika michuano mikubwa ya Ulaya msimu ujao.
Mahrez amekuwa akiwaniwa na Arsenal, Barcelona na Manchester
United, mkataba wake wa sasa umebakisha miezi 18.
Wakati huohuo, klabu hiyo inapambana kumbakisha klabuni hapo
kiungo wao, N’Golo Kante ambaye dau lake la kumuuza ni pauni milioni 20.
Post a Comment