MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Ndanda FC
ya Mtwara na Yanga SC imerudishwa nyuma kwa siku moja na sasa itachezwa Mei 14,
2016 badala ya Mei 15, 2016 kama ratiba ya awali inavyosomeka.
Taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) imesema sababu za kurudisha nyuma mchezo huo Na. 218 utakaofanyika Uwanja
wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara ni kuipa timu ya Young Africans nafasi ya
kujiandaa na kusafiri kwenda nchini Angola kwenye mchezo wa kimataifa wa Kombe
la Shirikisho Barani Afrika.
Mbali ya mechi hiyo, kuna michezo miwili ambayo imesogezwa
mbele kwa siku moja. Mechi hizo ni kati ya Simba na Mwadui ambayo sasa
itachezwa Mei 8, 2016 badala ya Mei 7, 2016.
Sababu za mchezo huo kusogezwa mbele ni kwamba Mei 7, 2016
kutakuwa na mchezo wa kimataifa utakaozikutanisha Yanga dhidi ya Sagrada
Esperanca ya Angola kuwania Kombe la Shirikisho.
Mchezo mwingine uliosogezwa mbele ni kati ya Kagera Sugar
dhidi ya Azam FC ambao sasa utafanyika Mei 8, 2016 badala ya Mei 7, 2016.
Sababu za mchezo huo kusogezwa mbele ni Uwanja wa Kambarage
Shinyanga. Mei 7, 2016 uwanja huo utakuwa na mchezo kati ya Stand United ya
Shinyanga dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Kadhalika Ligi Kuu Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea
kesho Mei 3, 2016 kwa mchezo mmoja ambao Yanga itakuwa mgeni wa Stand United
kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Jumatano Mei 4, 2016 Azam FC ya Dar es Salaam itakuwa
mwenyeji wa JKT Ruvu ya Pwani kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi nje kidogo ya jiji
la Dar es Salaam.
http://tanzaniabettingarena.blogspot.com
RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI
Post a Comment