MAREFA kutoka nchini Madagascar watachezesha mchezo wa
marudiano wa mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho
Afrika kati Sagrada Esperanca na Yanga SC ya Tanzania Mei 17, mwaka huu Uwanja
wa Sagrada Esperanca, zamani Quintalao do Dundo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) marefa
hao ni Hamada el Moussa Nampiandraza atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na
washika vibendera Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina.
Hata hivyo, CAF bado haijateua marefa wa kuchezesha mechi ya
kwanza baina ya timu hizo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Mei 7.
Yanga imeangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya
makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16
Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya
1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
Yanga ilianza vizuri kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya
Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla
ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na
kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Kwa upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali
waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa
2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani.
Katika Raundi ya kwanza wakaitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa
jumla ya mabao 2-1 ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na
kwenda hatua ya 16 Bora, ambako waliitoa V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya
mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.
CHANZO: BIN ZUBERY
Post a Comment