BAADA ya Yanga kumsajili Hassan Ramadhan Kessy, beki wa
kulia wa kikosi hicho, Juma Abdul, amesema kuwa hana shaka na nafasi yake
kwenye timu hiyo na badala yake anamkaribisha mwenzake huyo ili kuongeza changamoto kwenye kikosi chao.
Abdul amesema kuwa ujio wa Kessy ndani ya kikosi chao
utaongeza ushindani mkubwa kwani kila
mmoja anao uwezo na kocha ndiye atakayeamua.
“Sina shaka kabisa na ujio wake, naamini yeye ni mchezaji
kama mimi na mpira ni kazi yake, hivyo namkaribisha kwa furaha kwani naamini
kuna vitu atakuwa navyo ambavyo vitanisaidia mimi pamoja na timu kwa
ujumla.
“Naamini Kessy ni
mchezaji anayejua nini anafanya uwanjani, hivyo kuja kwake Yanga kutaongeza
ushindani wa namba jambo litakaloweza kujituma zaidi kwetu na hivyo kuifanya
Yanga kuwa na beki bora zaidi,” alisema
Abdul.
Kessy amesajiliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili,
jambo linaloonekana kutishia nafasi ya Abdul ndani ya kikosi hicho lakini
mwenyewe haogopi changamoto hiyo.
Post a Comment