EVERTON imeona Manchester United inazubaa na hivyo imeamua kuingia mbele na kuweka mzigo mezani ikimtaka Mreno Jose Mourinho awe kocha wao msimu ujao.
Everton ambayo kwa sasa inasaka kocha mpya kuchukua nafasi ya Roberto Martinez atakayeonyeshwa mlango wa kutokea baada ya mchezo wake wa mwisho Jumapili imefanya mawasiliano na Mourinho ili kumtaka atue Goodison Park.
Wanaamini kwamba kitendo cha Man United kuchelewa kufanya uamuzi kuhusu kocha wao Louis van Gaal, kinawapa nafasi ya kumnasa Mourinho mwenye kiu ya kurejea Ligi Kuu ya England.
Ripoti zinafichua kwamba Mourinho anashika namba moja kwenye orodha ya makocha wanaosakwa na Everton, huku kocha mwingine katika mpango huo ni Ronald Koeman wa Southampton.
Simu zimepigwa kwa Mourinho na wakala wake Jorge Mendes kutoka kwa mabosi wa klabu hiyo ya Merseyside kuona uwezekano wa kocha huyo kurejea Ligi Kuu England msimu ujao na kwenda kuwanoa The Blues wa Liverpool.
Mourinho aliweka wazi dhamira yake ya kurudi kwenye Ligi Kuu England na Everton ambao watakuwa na pesa za kutosha kufanya usajili mwaka huu wamekaa mstari wa mbele kumnasa Mreno huyo.
Man United haijielewi kama impige kibuti Van Gaal au endelee kubaki naye kikosini baada ya kuwafikisha fainali ya Kombe la FA msimu huu.

Post a Comment

 
Top