MSIMU wa 2015/16 wa Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ unafikia tamati wikiendi hii, lakini upande wa timu itakayotwaa ubingwa, hukumu inatarajiwa kutolewa leo, ambapo vigogo wawili wa ligi hiyo watakuwa uwanjani kuamua nani anakuwa bingwa.
Barcelona ina pointi 88 na Real Madrid ina pointi 87, zote zimebakisha mechi moja tu.
Barcelona inahitaji ushindi wa aina yoyote itwae ubingwa ambapo watakuwa wakikipiga dhidi ya Granada kwenye Uwanja wa Carmenes. Real Madrid nao watakuwa kwenye Uwanja wa Riazor kuivaa Deportivo la Coruna, ikiwa Madrid itashinda kisha Barcelona kupoteza mchezo wake au kutoka sare basi ubingwa utatua Madrid.
Vigogo hao wamekuwa katika presha kubwa kwa kuwa Barcelona inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Real Madrid, michezo yote hiyo itachezwa muda mmoja, saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.


Ateltico Madrid nao watashuka dimbani leo kukipiga dhidi ya Celta Vigo, ikiwa watashinda hawatakuwa na nafasi ya ubingwa hata kama Barcelona na Real Madrid zitapoteza kwa kuwa italingana pointi na Barcelona kisha kwa kanuni za La Liga wataangalia matokeo ya timu hizo zilipokutana nani alikuwa mbabe.

Barcelona iliifunga Atletico mabao 2-1 katika mechi zote mbili za La Liga. Mbali na mbio za ubingwa, kuna ushindani wa kuwania tuzo ya mfungaji bora ‘Pichichi’ ambapo vita kubwa ni kati ya Luis Suarez wa Barcelona mwenye mabao 37 na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid mwenye mabao 33.

Wakati huohuo, katika Ligi Kuu ya England ‘Premier League’ nayo inatarajiwa kufikia tamati wikiendi hii ambapo mechi zote zitachezwa muda mmoja kesho Jumapili, ushindani mkali ni katika nafasi ya pili, tatu na nne.


Tayari Leicester City imeshakabidhiwa ubingwa, Tottenham Hotspur inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 70 itakuwa uwanjani kukipiga dhidi ya Newcastle United, Arsenal ina pointi 68 ipo nafasi ya tatu itacheza na Aston Villa, Manchester City ipo nafasi ya nne kwa pointi 65 itacheza na Swansea City huku Manchester United ikishika nafasi ya tano kwa kuwa na pointi 63.

Katika Premier napo kuna vita kubwa ya kuwania ufalme wa ufungaji bora ambapo wanaowania ni Harry Kane wa Spurs mwenye mabao 25, Jamie Vardy wa Leicester mabao 24 na Sergio Aguero wa Man City mabao 24.

Post a Comment

 
Top