AMA kweli
kufa kufaana! Marcus Rashford atapewa fursa ya kufanya mazoezi katika kikosi
cha timu ya Taifa ya England kufuatia kuumia kwa Danny Welbeck, taarifa
mbalimbali zimebainisha.
Awali baadhi
ya vyombo vya habari mwezi uliopita viliwahi kuripoti kwamba Rashford
hazingatiwi kuwamo kwenye kikosi kitakachoshiriki Euro 2016, lakini majeraha
mabaya ya goti ya Welbeck yamelifanya benchi la ufundi kukutana Jumanne ambapo
straika huyo wa Manchester United
alipoanza kujadiliwa.
Rashford
alitarajiwa kuanza kupewa nafasi ya kwanza msimu ujao na hivi karibuni
aliachwa kwenye kikosi cha U-21 kwa
ajili ya mashindano yaliyofanyika Toulon, Ufaransa. Mabadiliko hayo yatamweka
Rashford katika mazingira ya kuaminiwa na kupata uzoefu katika kikosi cha
kwanza cha timu ya taifa.
Pigo la
Welbeck ambalo litamweka nje kwa miezi
tisa, limezua mjadala wa safu ya ushambuliaji ya timu ya taifa ya
England. Bado inaonekana nafasi ya Rashford ni ndogo kuweza kushiriki katika
kikosi cha Euro 2016, lakini kupata nafasi ya kufanya mazoezi na timu ya taifa
na kuonekana katika mechi za kirafiki kunaweza kumsaidia.
Kinda huyo
mwenye umri wa miaka 18- tayari amefunga mabao saba katika michezo16
aliyoitumikia United, akianza msimu wake wa kwanza kucheza soka la kulipwa kwa
kishindo Februari dhidi ya Midtjylland FC.
Post a Comment