STAA wa Muziki wa R&B kutoka Marekani, Shaffer Chimere Smith ‘Ne-Yo’ juzi usiku alitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Bongo ambapo anatarajiwa kupiga shoo ya kihistoria kwa mara ya kwanza leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mratibu wa shoo hiyo iliyopewa jina la Jembeka Festival 2016, Sebastian Ndege alisema kuwa Ne-Yo macho na masikio kwa mashabiki sasa yameelekezwa katika shoo hiyo ambayo haijawahi kutokea jijini Mwanza.
“Ne-Yo amejipanga vya kutosha na shoo ya kesho (leo) itakuwa historia kwani ataipiga live kwa kutumia vyombo,” alisema Sebastian.
Katika shoo hiyo, staa wa Muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond naye atakuwepo kumsindikiza Ne-Yo huku mastaa kibao wa Bongo Fleva wakiongozwa na Nature, Mo Music, Baraka Da Prince, Ruby, Stamina, maua na wegineo watalitawala jukwaa.
Naye Meneja Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania ambao ni miongoni mwa wadhamini wa tamasha hilo, Matina Nkurlu alisema anafurahi kwa staa huyo kufika salama ndani ya nchi ya Tanzania sasa ni wapenzi tu wa burudani kukata tiketi kwa wingi ili waweze kushuhudia shoo hiyo.
“Ninafurahi Ne-Yo amefika salama na mashabiki wa burudani waendelee kukata tiketi kwa wingi kadri iwezekanavyo ili waweze kuja katika Uwanja wa CCM Kirumba hiyo leo na huduma mbalimbali kutoka Vodacom zitapatikana ndani ya uwanja huo,” alisema.  
Shoo hiyo pia imedhaminiwa na Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba inayoendeshwa na Global Publishers.  

Post a Comment

 
Top