LOUIS VAN GAAL amekiri Manchester United haitakuwa na mafanikio kama haitafuzu kwa Ligi ya Mabingwa, lakini ana ujasiri kwamba ataendelea kuwa kocha wa kikosi hicho.
Kipigo cha Jumanne iliyopita cha mabao 3-2 dhidi ya West Ham kinamaanisha kwamba Mashetani Wekundu hao wamepoteza nafasi ya nne kwa Manchester City.
Vijana wa Van Gaal sasa wanatakiwa kushinda mchezo wao wa Jumapili dhidi ya Bournemouth na wakiombea Man City ipoteze kwa Swansea kitu ambacho bado ni kigumu.
Kushindwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa kulisababisha kocha aliyepita David Moyes kupoteza kibaru chake miaka miwili iliyopita na uvumi umeenea kwamba huenda Mdachi huyo akafuata nyayo, huku hamu ya  kocha, Jose Mourinho kurudi kazini ikichochea uvumi huo.
"Wewe na wenzio mlishanifukuzisha kazi miezi sita iliyopita, kwa hiyo nimekuwa nikifanya kazi katika mazingira hayo kwa miezi sita na bado tupo kwenye mashindano,'' alisema Van Gaal. " Huwezi kusema kwamba hatumo.
"Tunaweza kushinda Kombe la FA. Wangapi wapo kwenye mbio hizo? Wangapi? Hilo nalo haitoshi?

"Kwa kweli, kama hatutafuzu hatutakuwa tumetimiza malengo yetu. Hiyo ni kweli kwa sababu  malengo yetu ni kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa.  Hilo ndilo lengo letu.
"Lakini tunacheza fainali ya Kombe la FA na tuko kwenye mbio za kufuzu Ligi ya Mabingwa kwenye mchezo wa mwisho-  kimahesabu bado tunaweza kufuzu. Ni klabu ngapi zinaweza kusema hivyo?
"Bila shaka unaweza kusema Manchester United inahitaji kuwa mabingwa - kweli, Nafahamu, matarajio yalikuwa hayo, lakini sidhani kama hiyo ni hali halisi.
"Na nilishasema nitakuwepo hapa, hayo ni mawazo yangu, bodi inaweza kuamua kama ni hivyo. Hiyo ndiyo njia tofauti ya kwa kuiangalia hali halisi.''

Post a Comment

 
Top