Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea taarifa juu
ya mpango na kauli za baadhi ya viongozi wa Young Africans SC kushawishi
mashabiki wao kufanya vurugu dhidi ya warushaji matangazo ya televisheni ya moja
kwa moja wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika ngazi ya Makundi kati
ya Young Africans ya Tanzania na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) utakaofanyika Juni 28, 2016 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Dar es
Salaam.
TFF ikiwa msimamizi mkuu wa mpira
wa miguu Tanzania, inawajibika na mara moja inachukua nafasi hii
kuwatahadharisha baadhi ya viongozi wa Young Africans, wanachama na mashabiki
wao kutofanya hivyo kwani itakuwa ni kinyume na kanuni za mashindano na mikataba ya udhamini
katika hatua hii.
Ikumbukwe kwamba CAF inamiliki
asilimia mia moja ya haki za habari na masoko katika ngazi hii ya makundi na
jaribio lolote la kukwamisha matangazo ya biashara au utengenezaji na urushaji
wa matangazo ya televisheni au ukwamishaji wa shughuli zingine kama hizo kwa
CAF au wakala aliyeteuliwa na CAF kutaigharimu klabu mwenyeji si kwa kutozwa
faini tu lakini pia uwezekano wa kuondolewa mashindanoni.
Pia TFF inatoa tahadhari hiyo ikiwamo
ile ya utamaduni wa kukaa uwanjani ili kuepusha aina yoyote ya vurugu kwenye
michezo yake hususani hii ya hatua ya makundi. TFF inafahamu kuwa tayari
viongozi wa Young Africans walikwisha kusoma nyaraka na taarifa mbalimbali
kuhusu kanuni na masuala ya udhamini kwa timu zinazofuzu hatua ya Nane Bora.Wapenzi
wa Yanga wanaombwa kufika kwa wingi na kuishangilia kwa nguvu timu yao ikiwa ni njia ya kuitia hamasa.Hata
hivyo shamrashamra hizo zifanyike kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu za
Mpira wa Miguu na sheria za nchi.
Vitendo vya kuashiria vurugu na
kufanya vurugu vikithibitishwa katika taarifa ya Mwamuzi, Janny Sikazwe wa
Zambia; Kamishna wa mchezo, Celestin Ntangungira wa Rwanda na Mratibu Mkuu
Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza, hatua zake zitachukuliwa dhidi
yake ikiwamo KUONDOLEWA KWENYE
MASHINDANO. Vilevile vitendo vya kutishia amani,kudhuru mwili au kuharibu
mali vitachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za kijinai.
Katika mchezo huo wa kimataifa
Na. 107, Mwamuzi Sikazwe atasaidiwa na Jarson Emiliano dos Santos kutoka Angola
atayekuwa kwenye mstari wa kulia (line 1) na Berhe O’Michael wa Eritrea
atayekuwa upande wa kushoto (line 2) huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni
mwamuzi wa akiba.
Wakati huohuo, kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu nchini kinatarajia kukaa siku ya Jumamosi tarehe 2 Julai 2016. Taarifa
zaidi itatolewa karibuni.
…………………………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA
Post a Comment