BEKI wa kulia wa Yanga, Hassan Kessy, ametamka kuwa kambi
yao ya nchini Uturuki, anaamini itamfanya aongeze kiwango chake na kuwa na
makali zaidi kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.
Yanga kwa sasa ipo nchini Uturuki kwa kambi ya muda kabla ya
kwenda Algeria kucheza mechi yao ya kwanza ya hatua ya makundi katika Kombe la
Shirikisho Afrika dhidi ya MO Bejaia.
Kessy ambaye naye yupo kambini huko sambamba na nyota
wengine wanne waliosajiliwa na Yanga hivi karibuni, Juma Mahadhi, Andrew
Vincent ‘Dante’ na Beno Kakolanya, alisema kuwa nafasi ya kusafiri na kikosi
aliyoipata itamfanya kumuongezea namna ya kuwasoma zaidi wenzake ili siku ya
mechi ikifika asiwe kama mgeni.
“Kwa upande wangu nina furaha kuona kwamba nimesafiri na
kikosi licha ya kuwa ndiyo kwanza nimeingia hivi karibuni, lakini jambo hilo
linaonyesha kwa kiasi gani benchi la ufundi lilivyo na imani na mimi, niseme tu
kuwa sitawaangusha.
“Naamini kwa kupitia kambi hii ya Uturuki nitaweza kujifunza
mambo mengi ya Yanga ikiwemo mbinu, aina ya uchezaji na mambo mengine ambayo
yatanifanya nizidi kukiboresha kiwango changu na nina uhakika mara baada ya
kambi hii, nitakuwa moto zaidi na nitaisaidia timu yangu kufanya vizuri katika
michuano ya Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu Bara msimu ujao,” alisema Kessy.
Post a Comment