KOCHA Laurent Blanc ameachana na Paris Saint-Germain baada ya kukubaliana Malipo ya EURO Milioni 22 (£17m) kama ‘Kiinua Mgongo’ kwa Mujibu wa Gazeti la Michezo la Ufaransa L'Equipe.
Blanc alionekana yuko mashakani huko PSG tangu Wiki 3 zilizopita pale Rais wa Klabu hiyo Nasser al Khelaifi alipoelezea kuwa Msimu wao wa 2015/16 ulifeli kwa sababu ya wao kutupwa nje ya UEFA CHAMPIONS LIGI na Manchester City kwenye Hatua ya Robo Fainali.
Lakini, Nyumbani kwao France, PSG walifanikiwa kutwaa Trebo kwa mara ya Pili mfululizo walipobeba Ubingwa wa Ligi 1, Kombe la France na Kombe la Ligi.
Hata hivyo, kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI, PSG wamekuwa wakigota mwamba Hatua ya Robo Fainali kwa Misimu Minne mfululizo.
Blanc, Beki wa zamani wa France alietwaa Kombe la Dunia Mwaka 1998 na ambae pia aliwahi kuifundisha Timu ya Taifa ya France, alishika wadhifa PSG Mwaka 2013 baada ya Carlo Ancelotti kuondoka.
Blanc aliichezea Manchester United kwa Miaka Miwili na kufikisha Mechi 75 kati ya 2001 na 2003.
Blanc alisaini nyongeza ya Mkataba na PSG Mwezi Februari lakini, L'Equipe limesema ameondolewa PSG tangu Jana Jumatano huku ripoti zikiibuka kuwa Kocha wa Klabu ya La Liga huko Spain Sevilla, Unai Emery, ndie atashika wadhifa hapo PSG.


Post a Comment

 
Top