WACHEZAJI wawili wapya wa Yanga, Juma Mahadh na Obrey Chirwa
jana waliichezea Yanga kwa mara ya kwanza na kuonyesha kiwango cha kushtua
wengi.
Chirwa, raia wa Zambia ambaye alisajiliwa hivi karibuni
akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, aliitumikia Yanga kwa mara ya kwanza jana
kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo wa hatua ya makundi ya Kombe la
Shirikisho Afrika, akicheza namba kumi ambapo alionyesha kiwango cha juu.
Mchezaji huyo ambaye alishangiliwa na mashabiki wa Yanga
mwanzoni tu baada ya mchezo kuanza baada ya kukimbia na mpira, alionekana mara
kwa mara akipambana kuhakikisha anaipa timu yake ushindi lakini ikashindikana.
Hata hivyo, dakika ya kumi Chirwa alipiga kichwa safi,
lakini kama siyo umakini wa kipa wa Mazembe, Sylvain Gbhouo mambo yangekuwa
mazuri kwa Yanga.
Mchezaji huyo aliyeonyesha uzoefu wa kutosha alidumu
awanjani hadi dakika ya 71 ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Anthony Matteo.
Lakini ukiachana na huyo gumzo kuu jana lilikuwa kwa kiungo
Mahadh aliyetokea Coastal Union ambaye alizua mjadala mkubwa sana wakati wa
mapumziko baada ya mashabiki kuanza kujadili kiwango chake.
Dakika 15 za mwanzo alionekana kuwa na kasi nzuri huku
akitengeneza kona mbili ambazo hazikuzaa matunda.
Pamoja na kucheza kama mchezaji mwenye uzoefu, Mahadh
aliibuka tena katika dakika ya 55 ya mchezo ambapo alijaribu kuipenya ngome ya
timu hiyo lakini akachezewa madhambi.
Hata hivyo katika dakika ya 66 mchezaji huyo aliumia baada
ya kudondoka mwenyewe wakati akiwania mpira na beki wa Mazembe, ambapo
alitibiwa lakini baadaye alitolewa na kuingia Geoffrey Mwashiuya.
Hata hivyo, dakika walizocheza uwanjani wachezaji hao zimeonyesha
kuwa kocha wa timu hiyo hakukosea kuwasajili kwenye kikosi chake.
Post a Comment