China ni nchi ambayo inajengwa kwa dhamira. Wakidhamiria kufanya kitu fulani, watafanya kila linalowezekana kufanikisha. Ni miongoni mwa mataifa ya watendaji. Wanaongea lakini huku wanaongea,wanatenda. Waliwahi kudhamiria kuwa miongoni mwa mataifa yenye nguvu ya kiuchumi dunia. Leo sote tunajua wapo wapi.
Hivi sasa China wamedhamiria kuja kuchukua ubingwa wa soka duniani kwa maana ya Kombe la Dunia la Soka (Soccer World Cup). Ni dhamira na dira ambayo inaungwa mkono na Rais wao Xi Jinping ambaye ni mpenzi wa mpira toka utotoni.
Zipo nukuu ambazo zinasema Rais Xi Jinping aliwahi kusema mojawapo ya ndoto zake kuu ni kuona China ikiwa mwenyeji wa Kombe la Dunia na hatimaye kushinda kombe hilo. Mpaka hii leo China iliwahi kushiriki katika fainali za Kombe La Dunia mara moja tu. Ilifanya hivyo mwaka 2002 wakati michuano hiyo ilipofanyikia Korea Kusini na Japan. China walitoka kapa bila kufunga hata goli moja.
Miaka miwili iliyopita serikali ya China ilitangaza kwamba soka ni sehemu ya mitaala mashuleni. Hivi sasa wapo katika programu za kujenga viwanja na programu za mafunzo ya soka katika shule zaidi ya elfu ishirini (20,000). Miradi na programu hizo zinalenga katika kuibua wachezaji wapya wa soka zaidi ya 100,000 na ambao watajikita katika kuiletea China hiyo heshima inayoisaka.
Mbali ya programu hiyo ya kiserikali na bila shaka kwa shule za serikali, zipo shule binafsi ambazo zinaelekea kufuata mkondo huo. Mojawapo ni Evergrande Football School(sisi tunaziita hizi Academy). Shule hii iliyopo Qingyuan, Guangdong,China (Kusini mwa China) ndio Football Academy kubwa kuliko zote ulimwenguni. Ilifunguliwa rasmi mwaka 2012.
Shule ya Evergrande Football School inavyoonekana kwa juu. Ina ukubwa wa ekari zaidi ya 300 |
Mbali ya soka, wanafunzi wanasoma pia masomo ya kawaida ya darasani kama Kiingereza, Hesabu nk. Mwaka huu China imeongeza soka kuwa miongoni mwa vigezo vinavyoweza kutumika wakati wa mitihani ya kuingilia chuo kikuu. Nia ni kuwashawishi wazazi kwamba soka sio kikwazo kwa watoto wao kimasomo bali kitu chenye kuweza kuwa na faida kubwa maishani mwao.
Sanamu mfano wa Kombe la Dunia ambalo limewekwa nje ya shule hiyo kuwakumbusha wanafunzi kuhusu malengo ya jumla na muda mrefu-Kubeba Kombe La Dunia |
Kutokana na ushirikiano wa shule hiyo na Real Madrid, superstars kama Christiano Ronaldo na timu nzima ya Real Madrid hufanya ziara katika shule hiyo ili kuwatia moyo wanafunzi. |
Ni uhusiano ambao unajaribu kupeleka China uzoefu wa kisoka kutoka Hispania na hususani klabu ya Real Madrid. Ni mradi uliogharimu zaidi ya dola $185 bilioni. Shule au mradi huu ulijengwa kwa miezi kumi tu.
Post a Comment