AKIWA
na siku tatu tu mazoezini, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm amesema straika
wake mpya, Obrey Chirwa ameonyesha uwezo mkubwa na amefurahishwa kwani kasi ya
ufungaji mabao kwa timu yake imeongezeka.
Pluijm raia wa Uholanzi ameliambia Championi
Jumamosi kutoka kambini Antalya, Uturuki kwamba: “Nimefurahishwa na
kombinesheni ya Donald Ngoma na Chirwa, ana siku chache lakini ameniridhisha.”
Chirwa aliwasili Antalya, Jumatano iliyopita
na kujiunga na kambi hiyo maalum ya kujiandaa na mechi ya Kombe la Shirikisho
Afrika dhidi ya TP Mazembe itakayochezwa Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Chirwa ni raia wa Zambia aliyesaini mkataba wa
miaka miwili kuichezea Yanga akitokea FC Platinum inayoshiriki Ligi Kuu ya
Zimbabwe.
Pluijm alisema tangu mshambuliaji huyo ajiunge
na kikosi hicho huko Uturuki, amekuwa akimchezesha sambamba na Ngoma raia wa
Zimbabwe na ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga na kutoa pasi za mabao.
Chirwa anaandaliwa kucheza na Ngoma kwani
Amissi Tambwe raia wa Burundi ambaye hucheza na Ngoma, hatocheza dhidi ya TP
Mazembe kwa kuwa anatumia adhabu ya kadi mbili za njano.
“Nafurahia kuona Chirwa akicheza kwa kufuata
ninavyotaka ndani ya uwanja, anacheza soka la pasi za haraka, hapigi pasi za
nyuma akiwa na mpira pia ana uamuzi wa haraka anapofika kwenye eneo la hatari
la adui na anapiga mashuti makali.
“Nafarijika kuona muunganiko wa Ngoma na
Chirwa ukiimarika haraka ndani ya muda mfupi, hii inapunguza presha ya kumkosa
Tambwe.
“Naona mwanga wa kupata mabao mengi zaidi
katika mechi zetu tofauti na awali, sijapata ugumu sana kuandaa kombinesheni
hii inayocheza kwa kuelewana, Ngoma na Chirwa wamewahi kucheza pamoja FC
Platinum, siyo siri ninajisikia faraja mno.
“Mwanzo nilihofu Chirwa kuzoea mfumo wangu,
lakini alivyokuja akazoeana na wenzake na kushika kwa haraka,” alisema Pluijm.
Tambwe ndiye mfungaji bora wa msimu uliopita
wa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 21 wakati Ngoma alifunga mabao 17. Katika
michuano ya Caf, Ngoma ana mabao matatu na Tambwe analo moja.
Yanga imemsajili Chirwa akiwa chaguo la pili
baada ya kushindwa kumnasa straika Danny Phiri ‘Deco’ wa Chicken Inn ya
Zimbabwe. Chaguo la tatu alikuwa ni Walter Musona pia wa FC Platinum.
Post a Comment