MKWASA |
KOCHA wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema anatamani
kumtumia nahodha na beki wa kati wa zamani wa timu hiyo, Nadir Haroub
‘Cannavaro’ lakini hawezi kumlazimisha baada ya kukataa.
Cannavaro hivi karibuni alitangaza kustaafu kuichezea Taifa
Stars ikiwa ni siku chache tangu anyang’anywe cheo cha unahodha na kupewa
mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgji, Mbwana Samatta.
Beki huyo baada ya kunyang’anywa cheo hicho haraka
alitangaza kustaafu kuichezea Taifa Stars na kubaki na klabu yake ya Yanga
iliyotinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Mkwasa alisema yeye
alikuwa akihitaji uzoefu mkubwa alionao Cannavaro wa kucheza mechi nyingi za ya
kimataifa, hivyo anaamini angekuwepo kikosi chake kingeimarika.
CANNAVARO |
“Nilikuwa nahitaji uzoefu wa Cannavaro katika timu, lakini
kutokana na yeye mwenyewe kuamua kukataa kujiunga nasi, nimeona nimuache
nisiendelee kumlazimisha.
“Mimi sina taarifa za yeye kustaafu na hata hiyo barua
aliyosema ameandika haijanifikia, hivyo nimeamua kumuacha, wapo vijana wengine
nitakaowatumia,” alisema Mkwasa.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine
Mwesigwa, akizungumzia hali hiyo, alisema: “Hatujapokea barua ya Cannavaro
kustaafu kuichezea Taifa Stars, ndiyo maana aliitwa.”
Lakini Cannavaro alipotafutwa alisema: “Barua nimewapelekea
siku nyingi tu na nasisitiza kuwa nimestaafu kuichezea Taifa Stars.”
Mkwasa alimuita Cannavaro ili aichezee Taifa Stars mechi ya
leo dhidi ya Misri ya Kundi G kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon),
lakini beki huyo amegoma.
CHANZO: CHAMPIONI
Post a Comment