MCHEZAJI
wa TP Mazembe akitoa pasi ya bao analipwa dola 10,000 na atakayefunga pia
anapata kiasi hicho na timu ikishinda wachezaji wote wanapewa bonasi ya dola
5,000 kila mmoja katika mechi za kimataifa.
Dola 10,000 ni sawa na Sh milioni 21.8 na dola
5,000 ni sawa na Sh milioni 10.9, Yanga inayajua yote hayo ndiyo maana ikamtuma
beki wake wa zamani, Shadrack Nsajigwa kwenda kuichunguza timu hiyo.
Sasa Nsajigwa ameshafanya kazi yake na ametuma
barua pepe yaani e-mail kwa kimombo kwenda kwa Kocha wa Yanga, Hans van Der
Pluijm na sasa inafanyiwa kazi kambini Antalya, Uturuki.
Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro ameliambia Champoni
Jumamosi kuwa, tayari kocha ameipata ripoti ya Nsajigwa na sasa anaifanyia
kazi na kwa kiasi kikubwa mambo yataenda sawa.
“Ni kama kila kitu cha TP Mazembe tunacho
kwenye kiganja hivyo mashabiki wasiwe na wasiwasi kwani Nsajigwa ameifanya kazi
yake kwa ufanisi mkubwa na sasa kocha anaifanyia kazi ripoti yake,” alisema
Muro.
“Hatuwezi kuyataja mambo aliyotuletea Nsajigwa
lakini mashabiki wetu wanatakiwa kuamini kwamba tumeikamata TP Mazembe.”
Post a Comment