BEKI wa kati wa Yanga, Mtogo, Vincent Bossou, leo Jumatano anatarajiwa kujiunga na wenzake kwenye kambi yao huko Uturuki baada ya kukwama kwao nchini Ivory Coast.

Bossou ni mchezaji pekee wa Yanga ambaye bado hajajiunga na wenzake tangu walipopewa mapumziko ambapo imeelezwa kuwa alitakiwa ajiunge na wenzake tangu Jumatatu ya wiki iliyopita lakini kutokana na kukumbwa na matatizo ya kifamilia, ilibidi aendelee kubaki nyumbani kwao Ivory Coast.

Yanga ambayo imepiga kambi nchini Uturuki kabla ya keshokutwa Ijumaa kwenda Algeria kupambana na MO Bejaia kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirkisho Afrika, leo inafikisha siku ya tatu tangu itue nchini humo kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa Jumapili ya wiki hii.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, ameliambia Championi Jumatano kuwa, wana imani kuwa beki huyo atajiunga na wenzake leo Jumatano baada ya kumaliza matatizo yake ya kifamilia yaliyomkumba.

“Bossou tunatarajia kesho (leo) ajiunge na wenzake hapa Uturuki na hiyo ni baada ya kumaliza matatizo ya kifamilia yaliyomkumba.

“Lakini kwa upande wa kikosi kinaendelea vizuri na mazoezi na kimekuwa kikifanya mazoezi kila siku usiku kwa zaidi ya saa mbili huku pia hali ya hewa ikiwa ni murua kwetu kwani ni nyuzi joto 26 tu kama nyumbani Dar es Salaam.

“Tunatarajia Ijumaa ndiyo tuanze safari ya kwenda Algeria kucheza mechi yetu hiyo dhidi ya MO Bejaia, lakini kwa sasa wachezaji wote waliopo kambini wapo vizuri kiafya na hakuna mwenye tatizo lolote,” alisema Saleh.

Post a Comment

 
Top