KATIKA
mechi yake ya kwanza ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho Afrika wikiendi
iliyopita, wachezaji wa Yanga walionyeshwa sita za njano na nyekundu moja.
Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm amejiweka pembeni kwa kusema: “Nawaelekeza
kila siku lakini hawanisikii.”
Katika mchezo ulioisha kwa Yanga kufungwa bao
1-0 jijini Bejaia, Algeria, wachezaji watano walionyeshwa kadi hizo na mwamuzi
Janny Sikazwe na kupunguzwa kasi yao uwanjani.
Muda mwingi wachezaji wa Yanga walionekana
wakicheza kwa tahadhari kubwa wakiogopa kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na
nyekundu juu, hivyo kuidhohofisha timu.
Wachezaji walioonyeshwa kadi za njano ni Mbuyu
Twite, Simon Msuva, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Haji Mwinyi aliyeonyeshwa
mara mbili kisha kupewa nyekundu.
Mpaka sasa kwenye michuano ya kimataifa msimu
huu, Yanga imeshaadhibiwa mara mbili kwa kadi nyekundu ambazo ziliwakumba Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ na Mwinyi.
Pia wingi wa kadi za njano ukiwafanya Tambwe,
Ngoma na Thabani Kamusoko kukosa baadhi ya michezo muhimu tofauti.
Akizungumzia matukio ya wachezaji wake kupata
kadi hizo, Pluijm aliliambia Championi Jumamosi: “Kwanza huwa
siwafundishi wachezaji wangu kufanya madhambi au kuwalalamika waamuzi hovyo.
“Lakini pia katika mechi hizi za kimataifa
ambazo wachezaji wangu wamepewa kadi nyekundu, naweza kusema ile ya kwanza ya
kule Angola (dhidi ya Sagrada Esperanca), Cannavaro alionewa tu.
“Kadi nyekundu ya Mwinyi, inaonekana kama
alijitakia kwani bila ya ulazima wowote alimuingilia kwa nyuma mchezaji wa MO
Bejaia.
“Huwa nachukia sana kila ninapoona wachezaji
wangu wanapewa kadi ya aina yoyote ile kwani mazoezini huwa nafanya kila
linalowezekana kuwafundisha jinsi ya kuziepuka.”
Post a Comment