KOCHA wa Simba, Jackson Mayanja amesikia taarifa za
wapinzani wao, Yanga kusajili straika kutoka Zambia, Obrey Chirwa ambapo
ameupongeza usajili huo kwa kutoa sababu za kina lakini pia hakusita kutoa neno
baada ya kuibuka kwa taarifa za timu yake kumuwania straika Mrundi, Laudit
Mavugo.
Chirwa amesajiliwa hivi karibuni kwa kandarasi ya miaka
miwili akitokea FC Platinum ya Zimbabwe kwa ajili ya kuiongezea nguvu safu ya
ushambuliaji ya Yanga na kuziba pengo la Yousuf Boubacar wa Niger, aliyetemwa
kutokana na kiwango hafifu alichokionyesha msimu uliopita.
Akizungumza moja kwa moja kutoka kwao Uganda alikokwenda kwa
ajili ya mapumziko, kocha huyo alisema ni heri kama Yanga imeamua kuachana na
Boubacar ambaye hata yeye hakuona faida yake ikiwa anawekwa benchi na wazawa
hivyo ni bora wamemsajili Chirwa ambaye anasifika.
“Tukizungumzia soka halisi, Boubacar hakuwa na msaada kwa
Yanga maana kwa soka la Afrika Mashariki kama ni mchezaji wa nje katika kikosi
lazima uonyeshe kitu cha ziada kwa wazawa na kama hauna basi huna nafasi, sasa
kama Yanga wameamua kumuacha na kumchukua Chirwa hiyo ni safi.
“Naamini lazima watakuwa wameamuangalia kabla ya kufanya
uamuzi na zaidi kama ana msaada zaidi ya Boubacar basi hiyo ni safi na naamini
atawasaidia ingawa majibu zaidi yatapatikana akishaingia uwanjani.
“Kuhusu Mavugo nimesikia pia, lakini huyo siwezi
kumzungumzia zaidi maana ni mchezaji ambaye kama Mungu akipenda nitakuwa naye
msimu ujao, ningependa kumwangalia kwanza kabla ya kumzungumzia maana na mimi
sijawahi kumuona zaidi ya kumsikia tu,” alisema Mayanja.
Post a Comment