KUSTAAFU kwa Lionel Messi kuichezea
timu ya taifa ya Argentina, kumeigeuza nchi hiyo juu chini siku kadhaa
zilizopita, taifa lote likitetemeshwa na habari hizo baada ya Chile kuwafunga
tena kwenye fainali ya Copa America.
Rais wa Argentina, Mauricio Macri,
Meya wa Buenos Aires Horacio, Rodriguez Larreta na gwiji wa soka, Diego
Maradona, wamemwomba straika huyo wa Barcelona kubadili mawazo yake na huenda
ujumbe wote unaosambaa umekuja kupitia mwalimu wa Entre Rios, Yohana Fucks.
Ombi lake limewagusa mamilioni ya
mashabiki wa Argentina ambao wanatamani sana Messi abadili wazo lake la
kustaafu soka la kimataifa.
Barua kamili kama inavyosomeka:
Kwako Lionel Messi,
Yawezekana usiisome barua hii. Lakini
naiandika, si kama shabiki wa soka lakini kama mwalimu wa Argentina, kazi
ninayoipenda kama unavyopenda ya kwako.
Ningeweza kukuandikia kuhusu vipaji vyako vya
kipekee katika mchezo maarufu nchini mwetu, furaha ninayopata kuwa na fursa ya
kuona kizazi cha soka na kwa bahati njema kabisa kukushuhudia ukifanya miujiza
dimbani hali kadhalika jinsi unavyokonga nyoyo za mataifa yote duniani.
Kuelezea hayo nitakuwa narudia mambo. Badala
yake nataka unisaidie kutatua changamoto kubwa kuliko uliyokabiliana nayo wewe.
Nataka unisaidie zoezi gumu la kurekebisha tabia za watoto ambao wanakuona kama
shujaa wa soka na mfano wao wa kuigwa.
Haijalishi ni kiasi gani nina mapenzi na
ubobezi katika kazi yangu, siwezi kupokea sifa nzuri sana kutoka kwa wanafunzi
wangu kama ninavyokukubali. Sasa wataona mfano wao wa kuigwa ukikata tamaa.
Nakuomba usiwaridhishe watu dhaifu; wale ambao
wamekasirishwa kwa kushindwa kutimiza ndoto zao maelfu ambazo walishindwa
kutimiza kama wachezaji soka, wale ambao wanazungumzia mapumziko kwa sababu ni
jambo rahisi kutendeka.
Unasikia hili kutoka kwa mwalimu, ambaye licha
baina yetu, lakini nashughulika na tabia za Argentina za kudhani kazi ya mtu
mwingine ni rahisi, kwamba kufunga magoli ni rahisi kama kujenga nyumba au
mustakabali kwa ajili ya mtu.
Ni mtazamo huo unaoangusha wengi au kuzusha
hoja za kijinga zikiambatana na dharau na jazba juu ya ufanisi wa wengine,
kuthamini ushindi tu na kuhesabu makosa kuwa ni kushindwa, makosa hayo hayo
ndiyo yanayotufanya tuwe watu na tuendelee kujifunza.
Tafadhali usiache soka, usiwafanye wachezaji
wangu waamini kwamba nchi hii inajali ushindi tu kwanza. Usiwaonyeshe kwamba
hata uwe umefanikiwa kiasi gani hutaweza kuwafurahisha wengi na usiwafanye
waamini kwamba wanaishi ili kuwafurahisha wengine. Usiwape ujumbe wa makosa, licha
ya kukabiliana na changamoto nyingi hadi umekuwa maarufu leo hii.
Iwapo mtu kama wewe, mwenye familia inayokuunga
mkono, ukiwa na utajiri na mashabiki wengi, huwezi, wataaminije kwamba wanaweza
kukabiliana na vita hizo nyingi usiku na mchana?
Siwaelezi ni jinsi gani Messi anacheza soka la
kuvutia, lakini maelfu ya mashuti aliyopiga kufanya mazoezi ya kupeleka mpira
katika kona ambayo kipa hawezi kufika. Nawaeleza kuhusu Messi anayepata maumivu
ya kuendelea kukimbiza ndoto zake; Messi ambaye kwa fedha zote alizonazo
amefanikiwa kuwasaidia watoto wenye mazingira magumu. Nawaambia kuhusu Messi
aliyepevuka; baba wa familia na anayefanya kazi muhimu duniani, mzazi mwema;
Messi ambaye anakosa pia penalti, makosa yetu ndiyo yanayotufanya tuwe wanadamu
na hii inadhihirisha kwamba mchezaji bora hukosea pia.
Usikate tamaa, usitupe fulana yenye rangi za
nchi yetu mbali nawe, fulana hii ya Argentina inatuwakilisha sote. Tafadhali
usiwafanye wanafunzi wangu kuamini kuwa wao ni watu wa kushindwa.
Wanafunzi wangu wanahitaji kuelewa kwamba
mashujaa, wawe ni madaktari, askari, walimu au wacheza soka, ni wale
wanaojitolea kwa ajili ya wengine hata wakijua kwamba hakuna anayewathamini au
kuthamini kile wanachotoa, lakini wakiamini kwamba ushindi utakuwa ni wa wote
na kushindwa kutakuwa juu yao wenyewe. Lakini pamoja na yote hawakomi
kuthubutu. Lakini pia wana ujasiri ndani yao, wanapopambana dhidi ya kushindwa
hata ulimwengu wote ukisema hatutashinda.
Na siku moja watafurahia ushindi mkuu,
watafurahia pamoja na changamoto zote walizokabiliana nazo.
Kila mmoja huzungumzia mpira, lakini naamini
moyo wako ni thabiti.
Post a Comment