IKIWA na straika wa Barcelona, Luis Suarez katika benchi, Uruguay imeaga michuano ya Copa America baada ya kufungwa bao 1-0 na Venezuela katika mchezo wa Kundi C juzi alfajiri.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Lincoln, Salomon Rondon aliifungia Venezuela bao pekee na kufikisha pointi sita hivyo kufuzu kucheza robo fainali ya michuano hiyo.
Uruguay haina hata pointi moja katika Kundi C kwani ilipoteza mechi ya kwanza dhidi ya Mexico kwa kufungwa mabao 3-1. Mechi yake ya mwisho itakuwa dhidi ya Jamaica Juni 14, mwaka huu.

Kocha wa Uruguay, Oscar Tabarez hakumjumuisha Suarez katika kikosi chake licha ya mchezaji huyo kuwepo benchi na kupasha misuli moto, ila hakupanga kumtumia.
Tabarez alisema: "Siwezi kumtumia mchezaji ambaye hayupo fiti kwa asilimia 100, Suarez alikuwa mgonjwa na taarifa ya daktari ilisema hivyo.”

Hata hivyo, Suarez alionyesha kutoridhishwa na hali hiyo na alipiga ngumi kuta za plastiki za benchi la timu yake baada ya kugundua hatocheza mechi hiyo.

Post a Comment

 
Top