Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe ameondoka jana saa tatu na nusu usiku kwenda jijini Harare, Zimbabwe kumalizana na Kocha Kalisto Pasuwa.
Hans Poppe ameondoka na ndege ya Shirika la Ndege la Fast Jet kwenda kukamilisha "wanachotaka Wanasimba".
Pasuwa sasa anakinoa kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe na Simba ilifanya naye mazungumzo ya awali kwa simu na taarifa zinaeleza yuko tayari kutua Msimbazi.
Pamoja na Pasuwa, tayari Simba imefanya mazungumzo na mshambuliaji Mzimbabwe ambaye imeendelea kumficha.
Hans Poppe amezungumza na Championi Jumamosi na kusema anakwenda Zimbabwe kwa mambo yake ya kikazi.
“Kweli ninakwenda kwa masuala yangu ya kikazi, lakini kama kutakuwa na nafasi kwani shida ni nini kuzungumza nao,” alisema.
Hans Poppe alisema Simba inaendelea kujiimarisha kwa kuangalia ambacho wanahitaji baada ya Kocha Jackson Mayanja kukabidhi ripoti.



“Sisi tunaangalia ripoti ya mwalimu na nini kinahitajika, kawaida tunafanya mambo kwa nidhamu kubwa,” alisema.
Simba wameamua kufanya mambo yao kimya kwa kuwa wamelalamika wachezaji wengi wa kigeni waliwaangusha mwishoni baada ya wengine kufanya makusudi kuwakwamisha mwishoni.
Hivyo kwa sasa usajili kwao limekuwa ni jambo la umakini mkubwa ili kuepuka kufeli tena.

CHANZO: CHAMPIONI GAZETI

Post a Comment

 
Top